Monday, April 13, 2009

Duniani kuna watu

Kuna watu duniani, watu hao wacha Mungu,
Wamejawa na imani, siyo watu wa majungu,
Hao ni watu makini, kizazi tangu na tangu,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, wanazo tabia njema,
Ovu hawalitamani, huiepuka dhulma,
Mwenyewe tawabaini, ni wenye matendo mema,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, hupenda kutenda haki,
Huwaoni asilani, ubaya wakishiriki,
Wao yao ni imani, kuutunza urafiki,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, wao hawana tamaa,
Wawapo madarakani, matendo yao hufaa,
Husifika mitaani, na nyota zao hung’aa,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, maendeleo hupenda,
Hujitahidi kazini, mafanikio kulinda,
Fitina huwa pembeni, kwa yale wanayotenda,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, tabia zao ni mbaya,
Sijui huwaza nini, kwa ushenzi uso haya,
Wao huwa wafitini, hutenda mambo mabaya,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, wala siyo wacha Mungu,
Wana chuki mioyoni, hupenda sana majungu,
Hukuweka mtegoni, uone dunia chungu,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, huendekeza uwongo,
Huvuruga majirani, na kupenda masimango,
Hawaipendi amani, bali chongo kwayo chongo,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, hawafai asilani,
Sijui kwa kitu gani, huridhika mioyoni,
Sijui wapewe nini, sijui wafanywe nini,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, matendo hawayapimi,
Watu hawa duniani, nimewapa beti kumi,
Kalamu naweka chini, mengine tena sisemi,
Duniani kuna watu.

6 comments:

 1. Namshukuru mungu kwa kutuumba tofauti. Kwani ni kweli kuna watu duniani wema na wakatili. Wasiojali maisha ya mtu mwingine, wasipenda maendeleo ya wengine. Kweli kuna watu duniani

  ReplyDelete
 2. Duniani kuna watu,
  waso na utu,
  wenye roho za kutu,
  jeuri tena tukutu.


  Duniani kuna watu,
  wa'lo na utukufu,
  maisha ya utakatifu,
  kamwe wa'so na bifu...
  Hawa wako wachache,
  ukweli nisiufiche,
  uongo niushinde,
  watu wanipende,
  niwe miongoni mwa wale waishio milele.


  Tofauti za watu,
  kipimo cha imani zetu.
  Wote tungekuwa sawa,
  hakuna ambacho kingeendelea,
  Mungu katupendelea,
  wanyama wengine mwajionea,
  hawawezi endelea,
  kwani wote wajifanania.

  ReplyDelete
 3. wow! bado sijaelewa mnaweaje kutunga shairi namna hii. Hongereni sana:-)

  ReplyDelete
 4. Kweli kabisa Kissima,
  Manenoyo ni hekima,
  Maana dunia nzima,
  Sawa hatuwezi kuwa.

  Yasinta furahi sana,
  Mashairi yakazana,
  Kwa usiku na mchana,
  Tungo tutawaletea.

  ReplyDelete
 5. Kazi kwelikweli,
  Ila kweli nafurahi,

  ReplyDelete
 6. Nitangulize pongezi, na hongera sijakosea
  kupata wako mpenzi, mke watudhihirishia
  nidhamu utaienzi, na heshima kujiletea

  narudi kwa mashairi, fani unayoiwezea
  Wengine twajitahidi, kiasi kukufikia
  Si haba hata hili, viwango linafikia

  Japo ni staili ya longi, bado lajisanua
  Na manjonjo yake mengi, wazole kufikishia
  .......nitamalizia

  Nakumbuza enzi zangu
  Narap kiutukutu
  Kutunga tungo tamu
  Haikuwa kazi katu
  Sijui nimezeeka,
  Au ndo sina mzuka?
  Kama hivi mdogo mdogo nitaibuka
  Tena kushusha vina
  Kurudisha yangu heshima,
  Mtu mzima
  Nilijawa na maujanja ya kikubwa
  Ndo maan mpaka sasa,
  Naota natunga, naadika,
  Mistari vina,
  Sema sasa muda sina,
  Coz nipo shule nasoma
  But leo napima,
  Uwezo wangu mi kwa vina,
  Kama bado nastahili heshima...

  ReplyDelete