Monday, April 13, 2009

Duniani kuna watu

Kuna watu duniani, watu hao wacha Mungu,
Wamejawa na imani, siyo watu wa majungu,
Hao ni watu makini, kizazi tangu na tangu,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, wanazo tabia njema,
Ovu hawalitamani, huiepuka dhulma,
Mwenyewe tawabaini, ni wenye matendo mema,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, hupenda kutenda haki,
Huwaoni asilani, ubaya wakishiriki,
Wao yao ni imani, kuutunza urafiki,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, wao hawana tamaa,
Wawapo madarakani, matendo yao hufaa,
Husifika mitaani, na nyota zao hung’aa,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, maendeleo hupenda,
Hujitahidi kazini, mafanikio kulinda,
Fitina huwa pembeni, kwa yale wanayotenda,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, tabia zao ni mbaya,
Sijui huwaza nini, kwa ushenzi uso haya,
Wao huwa wafitini, hutenda mambo mabaya,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, wala siyo wacha Mungu,
Wana chuki mioyoni, hupenda sana majungu,
Hukuweka mtegoni, uone dunia chungu,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, huendekeza uwongo,
Huvuruga majirani, na kupenda masimango,
Hawaipendi amani, bali chongo kwayo chongo,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, hawafai asilani,
Sijui kwa kitu gani, huridhika mioyoni,
Sijui wapewe nini, sijui wafanywe nini,
Duniani kuna watu.

Kuna watu duniani, matendo hawayapimi,
Watu hawa duniani, nimewapa beti kumi,
Kalamu naweka chini, mengine tena sisemi,
Duniani kuna watu.