Monday, March 30, 2009

ndugu hawa ndugu jama

ndugu hawa, lipi kwao huwa jema,
kuwa sawa, ahsante wakasema,
liso dowa, lililo kwao salama,
ndugu hawa, ndugu jama.

ukitowa, na tena bila kupima,
huzodowa, ingawa umejinyima,
huchafuwa, uonekane si mwema,
ndugu hawa, ndugu jama.

vile huwa, mioyo inawachoma,
wewe kuwa, kujaaliwa karama,
fanikiwa, wao tu watakusema,
ndugu hawa, ndugu jama.

wakipewa, bado huukosa wema,
sipopewa, bado watakusakama,
chuki huwa, japo mwenyewe walima,
ndugu hawa, ndugu jama.

husumbuwa, ya kwao yakishagoma,
mwema huwa, na sifa dunia nzima,
hukutowa, ili wapate kusema,
ndugu hawa, ndugu jama.

ndugu hawa, lipi kwao huwa jema,
imekuwa, kwangu leo ninasema,
nilitowa, nadhani natenda wema,
ndugu hawa, ndugu jama.

na ikawa, nikawa najituma,
najitowa, nikidhani ni hekima,
haikuwa, vibaya akanisema,
ndugu hawa, ndugu jama.

lipi huwa, jema na wakalipima,
ukitowa, wakiri hivyo daima,
haijawa, maana siyo lazima,
ndugu hawa, ndugu jama.

ndugu hawa, nimejifunza nasema,
sitokuwa, ni bora iwe lawama,
bora kuwa, ni bora tangu mapema,
NDUGU HAWA, NDUGU JAMA.

4 comments:

 1. Pole sana kwa yote. Lakini kitu kimoja nafurahi umegundua ya kuwa haya ndio maisha. Pia kumbuka wahenga wetu walisema:- TENDA WEMA NENDA ZAKO USINGOJE SHUKRANI DUNIANI HAPA. Mungu akubariki uzidi kuwa mwema. Pia mvumilivu.

  ReplyDelete
 2. Pole sana kaka,
  watu hawa patashika,
  hawataki kuona umefika.
  kwako kuhangaika,
  ndio wanaridhika.
  ki-hivi kamwe hatutofika.

  Amini utayashinda,
  kwa Mungu kila alo panga litaenda.
  watu hao zidi kuwapenda,
  ipo siku yatawashinda.

  ReplyDelete
 3. Ahsante sana Kissima,
  Manenoyo ni hekima,
  Sitoacha utu wema,
  Mola 'takavyojalia.

  Nawe ukitenda wema,
  Usiangalie nyuma,
  Ahsante wasiposema,
  Mola 'takukirimia.

  ReplyDelete
 4. Raha kweli yaani bado sijaelewa ni vp mnakuwa wepesi kutunga hizi beti. Mongu awalinde.

  ReplyDelete