Thursday, January 22, 2009

Vukani

Nasema wote vukani, sauti zisikieni,
Tokeni usingizini, inukeni vitandani,
Tufanye jambo fulani.

Nasema wote vukani, ujasiri onesheni,
Isiwe kama zamani, za utumwa fikirani,
Kwani hiyo ni zamani.

Nasema wote vukani, mbiu kubwa ipigeni,
Isikike milimani, hata huko mabondeni,
Wote wakusikieni.

Nasema wote vukani, jikwamue akilini,
Sisi si mahayawani, twajua twataka nini,
Tungali mapambanoni.

Nasema wote vukani, mama wote majumbani,
Utumwa ukataeni, utumwa wa kizamani,
Imara msimameni.

Nasema wote vukani, nyie daraja la chini,
Kunyonywa kakataeni, maana ni ushetani,
Unyonyaji upingeni.

Nasema wote vukani, wanafunzi mavyuoni,
Ubaguzi ondoeni, ule kwenye udhamini,
Msikubali jamani.

Nasema wote vukani, nyie wa maofisini,
Hujuma zizuieni, ufanisi ujengeni,
Fitina iepukeni.

Nasema wote vukani, ambao mnazo dini,
Kamwe wasiwarubuni, ikapungua imani,
Mkajenga ufitini.

Nasema wote vukani, bado tungali vitani,
Hakuna raha moyoni, bado tungali shidani,
Hebu tujikwamueni.

Nasema wote vukani, tusilale asilani,
Usingizi uacheni, huleta umasikini,
Nieleweni jamani.

Nasema wote vukani, isiwe kama zamani,
Mtalala hadi lini, mridhike mioyoni?
Vukani basi jamani.

Nasema wote VUKANI!

2 comments:

  1. Nimelipenda jina hili la jamvi la da Koero. Nikadhani nijaribu kuliandikia vijimistari viwili vitatu.

    ReplyDelete
  2. kazi nzuri nimekuwa muda mreu sasa nimetamani kusoma mashairi yako. leo nimefurahi sana

    ReplyDelete