Thursday, January 22, 2009

Vukani

Nasema wote vukani, sauti zisikieni,
Tokeni usingizini, inukeni vitandani,
Tufanye jambo fulani.

Nasema wote vukani, ujasiri onesheni,
Isiwe kama zamani, za utumwa fikirani,
Kwani hiyo ni zamani.

Nasema wote vukani, mbiu kubwa ipigeni,
Isikike milimani, hata huko mabondeni,
Wote wakusikieni.

Nasema wote vukani, jikwamue akilini,
Sisi si mahayawani, twajua twataka nini,
Tungali mapambanoni.

Nasema wote vukani, mama wote majumbani,
Utumwa ukataeni, utumwa wa kizamani,
Imara msimameni.

Nasema wote vukani, nyie daraja la chini,
Kunyonywa kakataeni, maana ni ushetani,
Unyonyaji upingeni.

Nasema wote vukani, wanafunzi mavyuoni,
Ubaguzi ondoeni, ule kwenye udhamini,
Msikubali jamani.

Nasema wote vukani, nyie wa maofisini,
Hujuma zizuieni, ufanisi ujengeni,
Fitina iepukeni.

Nasema wote vukani, ambao mnazo dini,
Kamwe wasiwarubuni, ikapungua imani,
Mkajenga ufitini.

Nasema wote vukani, bado tungali vitani,
Hakuna raha moyoni, bado tungali shidani,
Hebu tujikwamueni.

Nasema wote vukani, tusilale asilani,
Usingizi uacheni, huleta umasikini,
Nieleweni jamani.

Nasema wote vukani, isiwe kama zamani,
Mtalala hadi lini, mridhike mioyoni?
Vukani basi jamani.

Nasema wote VUKANI!

Wednesday, January 14, 2009

Msione kimya

Hiki kimya kimezidi,
Msidhani makusudi,
Sijaishiwa weledi.

Wajibu naukumbuka,
Na sichoki kuandika,
Hata moyo kuridhika.

Nawakumbuka wenzangu,
Nawaombea kwa Mungu,
Ninyi ni rafiki zangu.

Na bado tupo pamoja,
Bado tunajenga hoja,
Tuna nguvu ya umoja.

Hatutochoka kwa sababu,
Hatujapata majibu.

Tuesday, January 6, 2009

Huba

Nijaze mie mahaba,
Ili nile nikashiba,
Nipe mapenzi ya huba,
Nitosheke na dunia.

Nipe chakula kitamu,
Kinijaze mi' wazimu,
Kinipandishe stimu,
Nibaki sikilizia.

Nigee mapenzi yote,
Yaniingie nidate,
Raha kamili nipate,
Raha isiyopungua.

Niambie wanipenda,
Siposema nitakonda,
Hata homa kunipanda,
Moyoni nikaumia.

Nifanye nifurahie,
Katu mi' nisiumie,
Mapenzi nijivunie,
Na raha kujisikia.

Nipe mimi peke yangu,
Usimpe na mwenzangu,
Umeumbwa uwe wangu,
Mungu amenipatia.

Kunipenda usichoke,
Wanifanya niridhike,
Na moyo uburudike,
U WANGU NAJIVUNIA.

Thursday, January 1, 2009

Mwaka Mwingine

Kabla hujafika wakati,
Nitaoshindwa toa sauti,
Nikashindwa vaa hata shati,
Nikakosa fikra madhubuti,
Macho yakapoteza saiti,
Ni vizuri ukanisikia.

Uianzapo siku nyingine,
Njema katika mwezi mwingine,
We' na wenzako mpongezane,
Kuufikia mwaka mwingine,
Tena na afya njema pengine,
Yakupasa kuifurahia.

Iwe furaha yenye kipimo,
Kuyatafakari yaliyomo,
Mwaka ulopita uwe somo,
Zidi tafuta bila kikomo,
Katika dunia uliyomo,
Naye Mungu atakujalia.

Lakini Mungu umshukuru,
Usifurahi kwa kukufuru,
Kesho akakunyima uhuru,
Wa kuiona nyingine nuru,
Ya bure hailipiwi ushuru,
Zingatia ninayokwambia.

Ni wengi sana waliopenda,
Kuzibadili zao kalenda,
Kwa bahati mbaya wamedunda,
Wakafunikwa ndani ya sanda,
Mungu apanga vile apenda,
Yeyote yule amchagua.


Heri ya Mwaka Mpya wa 2009 bloggers wote. Na wasomaji wetu wote.
One love.!