Sunday, December 21, 2008

U Rafiki Mwema

Mama ndicho kitu chema, nami leo ninasema,
Mama umejaa wema, nakiri hivyo daima,
'Menilea mimi vema, na leo mtu mzima,
Muhimu zote huduma, ulinipa hukupima,
Hata shule nikasoma, 'linifunza kujituma,
Niwe na tabia njema, kamwe nisirudi nyuma,
Mama u rafiki mwema.

U nguzo nayoegama, mambo yakiniandama,
Daima mwenye huruma, dunia 'kinisakama,
Wanijua mimi vema, sihitaji shika tama,
Wanifanya kusimama, zikinikumba zahama,
Wewe utafanya hima, kuona nipo salama,
Nikipatwa nayo homa, nitatibiwa mapema,
Mama u rafiki mwema.

Makosa nitaungama, nikitenda yaso mema,
Najua utayapima, tena ni kwayo hekima,
Wala hutoi lawama, mambo 'kienda mrama,
Umejaliwa karama, nakuombea uzima,
Mungu akupe neema, pamwe na afya njema,
Mimi nakupenda mama, na sitochoka kusema,
Mama u rafiki mwema.


Nimeandika shairi hili maalumu kwa mama yangu. Nakupenda sana mama. Na pia kwa akina mama wote, popote pale mlipo. Nawapongeza akina mama wote kwani mmetufanya tukawa hivi tulivyo. Mungu awabariki sana na kuwapa maisha marefu yenye furaha, amani na mafanikio.
Amina.

3 comments:

 1. leo ni leo!
  Ni kweli hakuna wa kufanana na mama. kwani mama ni mama.kwani mama, umekuwa tumboni mwake miezi sita na baada ya hapo amekulea , umwmuharishia na amekulea mpaka unakuwa mtu mzima. Kwa kweli hakuna mtu wa kufananisha kama mama. Na nawaomba wote ambao bado wana mama zao hai wawasikilize na kwatunza kwani hakuna/huwezi kubadili mama hata kama baba ameoa mke mwingie hakuna kabisa cha kufanananisha na mama. nafikiri wote mmenielewa!!

  ReplyDelete
 2. Jamani kusema kweli hakuna cha kufananisha kama mama. Mama ni mama. Napenda kuwaambia wote walio na mama kama hujamwambia mamako kuwa unampenda basi fanya sasa kwani ni muhimu sana.

  ReplyDelete
 3. Mama NI mamiyo, awe vyovyote awavyo, awe kilema, mfupi au mrefu bali vyovvyote awavyo umetoka tumboni mwake akakuleaukiwa tumboni kwa miezi tisa ukampa shida na kuchagua vyakula mbalimbali,hata baada ya kuzaliwa bado ukamnyonya na kumfanya anyong'onyee mara nyingine akose chakula cha kutosha kukunyonyesha,ukilia akubembeleza, ukiumwa akupeleka hospitali, mama halali hadi ahakikishe mwanaye kalala usingizi huku akimbembelezea nyoyo.

  Nasema hakuna kama mama wengine ni fotokopi anaye mdharau mama aje hapa nipambane naye nitamfirigisa hadi aone kilichomfanya awe na laana hiyo ya kummdharau mama yake.

  Wakatabahu

  ReplyDelete