Thursday, December 18, 2008

Nakuomba Mola Wangu

Nimechoka nimechoka, nimechoka peke yangu,
Mwenzenu nataabika, nahisi dunia chungu,
Nimechoka hangaika, namhitaji mwenzangu,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Nahitaji nami oa, kwani muda umefika,
Nimpate aso doa, mke alokubalika,
Niwe nayo njema ndoa, siyo ya kukurupuka,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Binti ntayempata, ajue kumcha Mungu,
Asiwe mwenye kunata, awe'shimu ndugu zangu,
Aitike nikimwita, hata mbele ya wenzangu,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Ajaaliwe nidhamu, nidhamu ya kwelikweli,
Ajawe na ufahamu, kufikiri mara mbili,
Hekima nayo muhimu, mazingira kukabili,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Sitaki mwenye kiburi, huyo ataniumiza,
Sitoitoa mahari, mwenye kukiendekeza,
Napenda ajidhihiri, hivyo asije nitweza,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Awe amefunzwa vema, awe na njema tabia,
Yawe maisha salama, asiruke na dunia,
Mola 'tatupa uzima, tutamtumainia,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Awe na uvumilivu, majira hayafanani,
Siku tukila pakavu, asizue tafrani,
Asitende jambo ovu, kuniweka matatani,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Sitochagua kwa dini, kabila ama kwa rangi,
Nitampenda moyoni, yeyote mi' simpingi,
Anifae maishani, ndilo jambo la msingi,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Na watoto tuwazae, Mungu akitujalia,
Tasa 'simnyanyapae, dunia kuichukia,
Kwa dhiki nikamfae, apate kujivunia,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Kuna kitu namwahidi, kwake nitakuwa mwema,
Sitofanya ukaidi, nitamw'eshimu daima,
Kwani kwake sina budi, kumwongoza kwa hekima,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Nitakuwa mwaminifu, kamwe sitomwumiza,
'Tamjali mara alfu, dhikini kumliwaza,
Na watu watamsifu, maana atapendeza,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Kaditama nimalize, kwa beti zangu dazeni,
Afaaye 'jitokeze, nimweke mwangu moyoni,
Mmoja tu nimtuze, huyo huyo maishani,
NAKUOMBA MOLA WANGU, NIPATIE MKE MWEMA.

4 comments:

 1. Fadhy, Hii ya leo ni mwisho. Ni sala nzuri sana nimefurahi sana, na nadhani mwenyezi mungu ameyasikia maombi yako. Kwani sio wengi wamwombao mungu awape mke mwema.
  Nami nakutakia umpate mke mweny hekima, upendo na pia awe mcha mungu na pia muwe mnaombeana katika maisha yenu.
  Nimeipenda sana sala hii.Ni hayo tu

  ReplyDelete
 2. Mke Mwema kumpata ni kudura za Mwenyezi,uombapo utapata muhimu ni kuwa wazi,wako wengi masalata na baadhi yao ni wezi,hujifanya wamepata, usiku hukumulika kurunzi.

  Maisha ya upweke si mema,muhimu kupata mwenzi,bali chunguza vyema, afaaye kukuenzi,tena muhimu kupima si wajua zama hizi?

  Kheri ninakutakia upate mke mwema, wa kukupa maliwaza, na kukuondolea majonzi, maisha pweke hukwaza,mtihani wake huviza.

  wakatabahu ndimi rafiki mwema

  ReplyDelete
 3. Niseme asante kabla ya hongera. Maana si sala yako pekee, bali ni fundisho pia. Yaani kwa wenye imani (yoyote) kumtegemea yule wamwaminiye katika kusaidia kupate kile wapendacho. Waonesha una nia, waonesha una subira, na waonesha uko tayari kwa yule atakayeletwa na huyo Umwaminiye. Nami nasema "your mental picture will determine your actual future".
  Again. Thanx alot for this GREAT POEM

  ReplyDelete
 4. Ahsante sana da Yasinta, kaka Mkwinda na kaka Mubelwa, maoni yenu si tu yamenipa faraja, bali pia yamenipa hamasa.
  Namwamini yeye aliye juu atanijaalia sawasawa na mapenzi yake.
  Amina.

  ReplyDelete