Tuesday, December 2, 2008

Msamaha

Hakuna alokamilika, sote tuna mapungufu,
Hutokea kengeuka, kwani si wakamilifu,
Binadamu hupotoka, huonesha udhaifu,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Usiogope kukosa, sote tumeumbwa hivyo,
Ni mtego tunanasa, vile tufikiriavyo,
Ama tukajenga visa, mengi t'watendeavyo,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Wala sione aibu, kuuomba msamaha,
Mwenye kukosa hutubu, wala si kukosa raha,
Neno zuri ndo wajibu, kwa kuitunza staha,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Samahani neno zuri, kwa wanaotuzunguka,
Tukosapo tukikiri, tunazidi heshimika,
Huo ndiyo ujasiri, tena usio na shaka,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Haifai ujeuri, haifai endekeza,
Ijenge yako nadhari, watu itawapendeza,
Wala siyo jambo zuri, wenzako ukawakwaza,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Makosa hurekebisha, zile tofauti zetu,
Msamaha huboresha, tuishivyo na wenzetu,
Upendo huimarisha, udugu kati ya watu,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Hakuna aliye mwema, kwa asilimia mia,
Wenzetu wakitusema, haipaswi kuwanunia,
Makosa yanatupima, uwezo kuvumilia,
PALE UNAPOKOSEA, BASI OMBA MSAMAHA.

10 comments:

 1. Fadhily! Neno samahani ni neno rahisi sana. Lakini inapofika ile dakika ya kusema SAMAHANI hapo ndo kasheshe. Kumwomba mtu samahani/radhi kwa makosa aliyofanya sijui kwa nini inakuwa ngumu sana. Hili jambo inabidi tulifanyie utafiti. Kwani bila hivyo tutakuwa tunaumia sana katika mioyo yetu na mwisho wake labda kupata vidonda vya tumbo. Ni muhimu sana kuombana radhi/msamaha mara moja tu tukosapo kama Fadhily alivyosema.

  ReplyDelete
 2. Da Yasinta, ni kweli watu tu wazito kuomba msamaha pale tunapowakosea wenzetu. Wengi tunadhani ukiomba samahani sijui utaonekana vipi?
  Lakini mimi naamini, 'kukiri udhaifu hakumdhoofishi mtu, bali kunamuimarisha.'
  Nimeandika shairi hili kwa sababu nimejifunza kuwa watu wengi huumizwa kwa matendo yetu, na huumizwa zaidi pale tunapoonesha hatujali pamoja na kwamba tumewafanyia makosa.
  Lakini kama tungezitumia sekunde chache tu, kusema, 'nakiri nimekosa, naomba msamaha.' Basi pengine mambo mengi katika maisha yetu yangekuwa tofauti na yalivyo sasa.
  Tunapaswa kuomba msamaha tukosapo, kwa sababu hatuwezi epuka fanya makosa.
  Nakushukuru sana da Yasinta kwa mchango wako, nauthamini pakubwa.
  Ubarikiwe sana.
  Alamsiki.

  ReplyDelete
 3. Nshakupata vyema,Nilikuona mapema, kwa fani umetuama,kazi zako zinasema, budi kuwa mtu mwema, kwa uzima na salama, nakutakia kazi njema, waisome watu wema,walo Mtwara na Kigoma, NDIMI rafiki mwema,Mkwinda ninayesema.

  Wakatabahu siku njema, hapa nimetuama

  ReplyDelete
 4. Nshakupata vyema,Nilikuona mapema, kwa fani umetuama,kazi zako zinasema, budi kuwa mtu mwema, kwa uzima na salama, nakutakia kazi njema, waisome watu wema,walo Mtwara na Kigoma, NDIMI rafiki mwema,Mkwinda ninayesema.

  Wakatabahu siku njema, hapa nimetuama

  ReplyDelete
 5. Ahsante ninaisema, kwako ee rafiki mwema,
  maoni nimeyasoma, yamesheheni hekima,
  zidi kuwa mtu mwema, wala usirudi nyuma,
  Mkwinda rafiki mwema.

  Tuombeane uzima, tuwe na afya njema,
  Tufanikiwe daima, kwenye mapito salama,
  Tuwe wenye kujituma, maana Mungu yu mwema,
  Mkwinda rafiki mwema.

  ReplyDelete
 6. Ningekuwa mkwinda ningejidai sana kuwa na rafiki mwema kama Fadhy. Kwani amakutungia shairi nzuri sana hata binti yangu amelipenda.

  ReplyDelete
 7. U rafiki mwema pia, ahsante sana dadangu,
  Nami ninafurahia, waja blogini kwangu,
  Huchoki nitembelea, kwenye mashairi yangu,
  Ahsante sana dadangu.

  Wala sijakubagua, kumpendelea Mkwinda,
  Marafiki mmekua, hivyo nyote nawapenda,
  Vichwa mnavisugua, kwa mada zisizopinda,
  Ahsante sana dadangu.

  Bintiyo mpe salamu, kheri ninamuombea,
  Afanikiwe dawamu, katika hii dunia,
  Mungu atamkirimu, hekima kumjalia,
  Ahsante sana dadangu.

  ReplyDelete
 8. Dah! Nadhani nahitaji ku-reboot u-malenga wangu nami nianze kumwaga "verses" humu. Inanoga saana kuona watu wanaweka mashairi kuanzia main page mpaka kwenye maoni.
  I Love This
  Blessings

  ReplyDelete
 9. Mzee wa changamoto, karibia uwanjani,
  Kipaji sawa na wito, wala 'siweke kapuni,
  Mwaga tungo motomoto, nasi tutoe maoni,
  Usikitupe kipaji.

  Shairi huleta hamu, kulisoma kwa madaha,
  Shairi ni tungo tamu, usomapo lina raha,
  Hupanua ufahamu, na kuongeza furaha,
  Usikitupe kipaji.

  Nafurahi kusikia, pia nawe mshairi,
  Siache kikapotea, tena siyo jambo zuri,
  Kipaji chako tumia, uwe mtunzi mahiri,
  Usikitupe kipaji.

  Karibu tena na tena, karibu pasi kuchoka,
  Hapa twashauriana, kwa yanayotuzunguka,
  Kwani sote tu vijana, tuendako tutafika,
  Usikitupe kipaji.

  ReplyDelete
 10. Kazi za Bwana Fadhili ni za kipaji na adili,zasomwa na wenye mali na wale waso na hili,zasomeka kulihali, tena kwa kutafakari.

  Fanya bila mushkeli, kalamuyo si dhalili,unene kwa njema kauli,ienziwe na aali,wajenena ja Fadhili, waambe nasi tu mahiri.

  Walikuwepo awali, wakanena kulihali, waneneje wanawali, wambuji wa zino hali, zisopata wenye mwili ela wa dhoofulhali,
  tamba kwa zino hali nasi tu washairi.

  Ndimi mnenaji wa hali, wa duni lmushkeli, maisha yaso na hali,Mkwinda mwenye adili,mfikishaji kauli

  ReplyDelete