Monday, December 8, 2008

Miaka 47: Twaweza kutabasamu?

Awali Bismillah, sifa zake Maulana,
Hii yangu istilahi, nimeifikiri sana,
Siitaki ikirahi, nifikiripo kwa kina,
Twaweza kutabasamu?

Twaweza kutabasamu? pengine ningeuliza,
Kama swali ni gumu, nani atayetujuza?
Nani ni lake jukumu, ukweli kutueleza,
Twaweza kutabasamu?

Hao wenye tamrini, kote wameshatandama,
Wengine waturubuni, maadili yanazama,
Wengine watufitini, twakosa pa kuegama,
Twaweza kutabasamu?

Twasema tupo huru, tena twasherekea,
Ni kweli na haidhuru, lakini tunaumia,
Twapata ufurufuru, ufisadi kuzidia,
Twaweza kutabasamu?

Viongozi wenye nia, tulonao ni wachache,
Wengine watuibia, akili zao macheche,
Nasi tunawaambia, tabia hizo waache,
Twaweza kutabasamu?

Wanaiba tena vyote, wanakuwa wajeuri,
Ili sisi tusipate, ila wao ufahari,
Yaani sisi tusote, ili wao washamiri,
Twaweza kutabasamu?

Uhuru ni kitu gani, labda tungefahamu,
Maisha yetu ni duni, viongozi wadhalimu,
Kufikiri wakunguni, bali wapenda takwimu,
Twaweza kutabasamu?

Kila tukitaradhia, inatubidi kusota,
Lini tunaingojea, maezi yetu kupata?
Wao hujizidishia, ila sisi tunagota,
Twaweza kutabasamu?

Kuhusu hayo madini, twasema kila uchao,
Mikataba wasaini, kujali nafsi zao,
Nchi yawa masikini, huku ukwasi inao,
Twaweza kutabasamu?

Uhuru wa kifikra, twahitaji utumia,
Fikra ziso marara, zenye kutusaidia,
Nchi yetu ikang'ara, ndicho tunategemea,
Twaweza kutabasamu?

Tuudumishe umoja, tuepuke ubaguzi,
Tusingoje siku moja, kwa wabovu viongozi,
Waondoke mara moja, kuwafuga hatuwezi,
Twaweza kutabasamu?

Twataka kutabasamu, twaihitaji sababu,
Sababu tena muhimu, uhuru uwe dhahabu,
Ili sote kwa kaumu, tuuenzi pasi ta'bu,
TWAWEZA KUTABASAMU?

4 comments:

 1. Uhuru ni kuwa huru,
  Kuweza kusema ulichonacho moyoni,
  N apia inabidi tuwe pamoja,
  na kama inawezekana tuwatoe viongozi wabovu, kwani hawaleti maendeleo yoyote, na kuna watu ambao wanaweza kuwa viongozi bora na kuleta maendeleo. Kwani kama tupo huru basi tuonyeshe kweli tupo HURU sio kukaa tu na kutabasamu wakati hakuna cha KUTABASAMU. Sijui kama nimeeleweka

  ReplyDelete
 2. Umeeleweka sana,
  Tena inawezekana,
  Vema kushirikiana,
  Wabovu kuwaondoa.

  Kwetu hawana maana,
  Wameshatunyonya sana,
  Twahitaji kukazana,
  Twahitaji kuwatoa.

  Tufikirie kwa kina,
  Tusifanye kama jana,
  Tusiwachague tena,
  Makosa tukarudia.

  Sote tutaambizana,
  Kwani tumechoka sana,
  Huku ni kudanganyana,
  TUMECHOKA VUMILIA.

  ReplyDelete
 3. Ni kweli inabidi kufikiria kwa makini, ili tusifanya makosa tena. Kuvumilia tuache kwani tunaumia tu.

  ReplyDelete
 4. Haya sasa. Luciano alisema "while we seaching for the solution, should we trust in GOD or Man? Should we keep on being the victims, while supporting the babylon systems? Let's revolts against all evils, so that our concious will be free. And fight if we have to....."
  Uhuru bila kuwa huru ndio dhana waitumiayo hawa waheshimiwa wanaotaka kujifanya wanafikiria pamoja kwa umoja kwa kutumua "common sense" ambayo haijawahi kuwa common.
  Wanatekenya jiwe na siku likicheka, watalia wao.
  Hatuna la kutabasamu maana baadhi ya sehemu ziko kwenye hali mbaya kuliko zilivyokuwa wakati nchi inapata uhuru. Sijui tafsiri ya uhuru kwa mwananchi wa huko ni ipi? Kwamba mnateswa na mTanzania mwenzako na si mtu-baki? Ama kuwa wakoloni walikuwa wakitujali kuliko tulivyo sisi? Ndio maana twafikia kujiuliza kama twataka kuwa "watumwa tulishwao vema ama watu huru tufao kwa njaa"?
  See you Next Ijayo

  ReplyDelete