Wednesday, December 10, 2008

Kila Jambo

Sifa ni zake Karima, yeye kaumba dunia,
Katupatia uzima, nasi twaufurahia,
Katujalia hekima, sasa twaitumia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Upo wakati wa heri, wakati wa mwambo pia,
Mambo yote kuwa shwari, ama kuharibikia,
Wakati wa kunawiri, ama kutanga na njia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Kuna wakati wacheka, siku zingine kulia,
Wakati wa kuridhika, ama mambo kuchachia,
Siku za kukubalika, ama za kukuchukia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Kupata nguvu kusema, ama kusikilizia,
Kunena kwayo hekima, ama bila fikiria,
Kupata yako heshima, kudharaulika pia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Kila utakachopanda, kumbuka kuvuna pia,
Kufanya unalopenda, ama kukuamulia,
Uhuru utakokwenda, ama wakakufungia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Leo wala na kushiba, kesho njaa kuingia,
Ukajaziwa kibaba, ama wakakuibia,
Ukapata mara saba, kuibiwa mara mia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Wakati wa kupokea, ujuwe kutowa pia,
Raha zikikunogea, juwa kuna kujutia,
Leo ukichekelea, kesho shida vumilia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Kuna siku za furaha, na siku zenye udhia,
Kuishi maisha raha, ama shida kuingia,
Ukashukiwa na jaha, ama kusota dunia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Utapata marafiki, kesho watakukimbia,
Utahimili mikiki, ama siku kuumia,
Utaikosa limki, ama kesho kukujia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Tena kuna kuzaliwa, kisha kuna kufa pia,
Kuna karama kupewa, na kushindwa itumia,
Afya njema ikawa, maradhi kukuingia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Ya kusema nimesema, najua mumesikia,
Nimeipata karama, haya nikawaambia,
Ninagota kaditama, ni lenu kufikiria,
MAMBO HAYA HUTOKEA, KILA JAMBO KWA WAKATI.

6 comments:

 1. Ni kweli inabidi kumshukuru mungu kila pumzi upumuayo,utembeapo, na kila kitu ufanyacho. Napia ni vizuri kumshukuru kwa kukupa marafiki na wewe kwa kuweza kutoa na kupokea toka kwa wengine.
  Fadhy, Je? maoni yangu yameeleweka

  ReplyDelete
 2. Yameeleweka da Yasinta, tena vizuri sana.
  Nimeandika shairi hili makusudi ili tukumbushane kuhusu haya mambo ya maisha.
  Pengine ningehitaji sentensi moja, "hujafa hujaumbika"
  maadamu tu duniani, shurti tuzikabili nyia za maisha.
  Ahsante sana kwa kunitembelea mara kwa mara. Naamini umelipenda shairi hili kama uyapendavyo mengine!
  Alamsiki.

  ReplyDelete
 3. yaani sana tu nimesoma mara saba mra sabini. ulijuaje kama nimelipenda au unajua kuagua pia. ha ha ha haaa.

  Ila uwongo mbaya nayapenda mashairi yako sana kazi nzuri sana. Nami napenda kukushukuru kwa kunitembelea daima. Usichoke kutembelea tena na tena

  ReplyDelete
 4. Nimejua mtani, si unajua tulivyo juu katika kubashiri!
  Ni vile najua wapenda kusoma mashairi. Nimefurahi sana kwa kuyapenda mashairi yangu.
  Kaka zangu nao naamini watalipenda.
  Naomba nirudie kusema ahsante sana.

  ReplyDelete
 5. Fadhy, Nimeona umekipamba kijiji chako kazi nziri mtani. kijiji kinapendeza. Wikiend njema nawe usisahau kusali

  ReplyDelete
 6. Ahsante sana kwa pongezi zako. Napenda mapambo ya kijiji chako.
  Ndo nimetoka church.
  Jumapili njema.

  ReplyDelete