Wednesday, December 31, 2008

Ahsante sana Mungu

Siku muhimu 'mefika,
Mwaka unamalizika,
Ni mbali tulikotoka,
Mola katupa baraka,
Ni wengi hawajafika,
Ahsante sana Mungu!

Eeh Mola tupe karama,
Tujalie yale mema,
Uzidi tupa uzima,
Mwaka uishe salama,
Mola mwingi wa Rehema,
Tunakushukuru sana!

Saturday, December 27, 2008

Karibu sana Yasinta

Karibu sana nyumbani, karibia Tanzania,
Sote tupo furahani, kwa hamu twakungojea,
Hakika twaitamani, siku hiyo kuwadia,
Karibu sana Yasinta.

Warudi kutoka mbali, mbali sana na nyumbani,
Twafurahi kila hali, nyumbani kupathamini,
Ukiwa mbali mahali, hujiona ugenini,
Karibu sana Yasinta.

Nyumbani jama pazuri, nyumbani panayo raha,
Mwenyewe hebu fikiri, nyumbani huwa furaha,
Ukifika utakiri, nyumbani siyo karaha,
Karibu sana Yasinta.

Yasinta tunakungoja, uzilete changamoto,
Yasinta mwingi wa hoja, tena hoja moto moto,
Kwetu u kama daraja, ili tuuvuke mto,
Karibu sana Yasinta.

Nyumbani usipachoke, maana panapendeza,
Hata kesho pakumbuke, usije kupatelekeza,
Tena pana raha yake, na tena tutakutuza,
Karibu sana Yasinta.

Karibu sana Yasinta, twakukaribisha sote,
Nyumbani utatukuta, nasi furaha tupate,
Na jasho tutakufuta, tunapaswa tukufute,
Karibu sana Yasinta.

KARIBU SANA NYUMBANI.

Sunday, December 21, 2008

U Rafiki Mwema

Mama ndicho kitu chema, nami leo ninasema,
Mama umejaa wema, nakiri hivyo daima,
'Menilea mimi vema, na leo mtu mzima,
Muhimu zote huduma, ulinipa hukupima,
Hata shule nikasoma, 'linifunza kujituma,
Niwe na tabia njema, kamwe nisirudi nyuma,
Mama u rafiki mwema.

U nguzo nayoegama, mambo yakiniandama,
Daima mwenye huruma, dunia 'kinisakama,
Wanijua mimi vema, sihitaji shika tama,
Wanifanya kusimama, zikinikumba zahama,
Wewe utafanya hima, kuona nipo salama,
Nikipatwa nayo homa, nitatibiwa mapema,
Mama u rafiki mwema.

Makosa nitaungama, nikitenda yaso mema,
Najua utayapima, tena ni kwayo hekima,
Wala hutoi lawama, mambo 'kienda mrama,
Umejaliwa karama, nakuombea uzima,
Mungu akupe neema, pamwe na afya njema,
Mimi nakupenda mama, na sitochoka kusema,
Mama u rafiki mwema.


Nimeandika shairi hili maalumu kwa mama yangu. Nakupenda sana mama. Na pia kwa akina mama wote, popote pale mlipo. Nawapongeza akina mama wote kwani mmetufanya tukawa hivi tulivyo. Mungu awabariki sana na kuwapa maisha marefu yenye furaha, amani na mafanikio.
Amina.

Thursday, December 18, 2008

Nakuomba Mola Wangu

Nimechoka nimechoka, nimechoka peke yangu,
Mwenzenu nataabika, nahisi dunia chungu,
Nimechoka hangaika, namhitaji mwenzangu,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Nahitaji nami oa, kwani muda umefika,
Nimpate aso doa, mke alokubalika,
Niwe nayo njema ndoa, siyo ya kukurupuka,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Binti ntayempata, ajue kumcha Mungu,
Asiwe mwenye kunata, awe'shimu ndugu zangu,
Aitike nikimwita, hata mbele ya wenzangu,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Ajaaliwe nidhamu, nidhamu ya kwelikweli,
Ajawe na ufahamu, kufikiri mara mbili,
Hekima nayo muhimu, mazingira kukabili,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Sitaki mwenye kiburi, huyo ataniumiza,
Sitoitoa mahari, mwenye kukiendekeza,
Napenda ajidhihiri, hivyo asije nitweza,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Awe amefunzwa vema, awe na njema tabia,
Yawe maisha salama, asiruke na dunia,
Mola 'tatupa uzima, tutamtumainia,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Awe na uvumilivu, majira hayafanani,
Siku tukila pakavu, asizue tafrani,
Asitende jambo ovu, kuniweka matatani,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Sitochagua kwa dini, kabila ama kwa rangi,
Nitampenda moyoni, yeyote mi' simpingi,
Anifae maishani, ndilo jambo la msingi,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Na watoto tuwazae, Mungu akitujalia,
Tasa 'simnyanyapae, dunia kuichukia,
Kwa dhiki nikamfae, apate kujivunia,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Kuna kitu namwahidi, kwake nitakuwa mwema,
Sitofanya ukaidi, nitamw'eshimu daima,
Kwani kwake sina budi, kumwongoza kwa hekima,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Nitakuwa mwaminifu, kamwe sitomwumiza,
'Tamjali mara alfu, dhikini kumliwaza,
Na watu watamsifu, maana atapendeza,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Kaditama nimalize, kwa beti zangu dazeni,
Afaaye 'jitokeze, nimweke mwangu moyoni,
Mmoja tu nimtuze, huyo huyo maishani,
NAKUOMBA MOLA WANGU, NIPATIE MKE MWEMA.

Nataka kusema kitu

Nataka kusema kitu, bado nakifikiria,
Nifikiri mara tatu, kisha nitawaambia,
Ninachotaka kusema.

Nimepatwa na ufyatu, mambo yamenizidia,
Msiotwe roho kutu, mwapaswa nisaidia,
Kuna kitu ntasema.

Miaka makumi tatu, mie naikaribia,
Nami kati yao watu, heshima naitakia,
Mwaelewa nachosema?

Na huu siyo upatu, nikaukurupukia,
Nitawashangaza watu, ovyo kujiamulia,
Niendelee kusema?

Moyo wangu siyo butu, pekee kujikalia,
Nao wahitaji kitu, kesho nitawaambia,
Basi kesho ntasema.

Monday, December 15, 2008

Alaa Kumbe!

Asubuhi waamka,
Waanza kukuna kichwa,
Unawaza,
Utawaza sana!
Ukipata jawabu,
Heko nyingi.

Jana,
Hukuyamaliza yalojiri,
Ungeyamaliza vipi?
Uwezo hukuwa nao,
Kwa nini?
Najua huna jibu.

Maisha!
Kwani ni nini?
Ama yana nini?
Utawaza sana,
Nami nawaza sana,
Ala kumbe?
Kumbe nini?

Wajiuliza mara mia,
Uwape tena?
Lipi jipya litakuja?
Ngoja kidogo.
Maisha, maisha,
Yanakwisha,
Usiseme hivyo,
Nisemeni?
Sijui.
Hayo madaraka,
Tumewapa,
Wengine wakachukua bila kupewa,
Nini chanzo?
Pengine tamaa.
Tulikuwa na matarajio,
Eti eh!

Matarajio?
Ya nini tena,
Kwenu hamli?
Hapana.
Sasa nini?
Hali bora.

Alaa kumbe!
Ikawaje sasa?
Hatuhitaji kukujibu,
Maana hali yenyewe,
Mwenyewe si unaiona?

Hapana sioni kitu,
Ni kweli,
Huoni kitu ingawa una macho,
Machoyo mapambo,
Huwezi ona lolote,
Kwa kuwa,
Hupendi kufanya jitihada,
Jitihada? Za nini tena?
Katika kufikiri.

Mmh!
Sote tukaguna.

Wednesday, December 10, 2008

Kila Jambo

Sifa ni zake Karima, yeye kaumba dunia,
Katupatia uzima, nasi twaufurahia,
Katujalia hekima, sasa twaitumia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Upo wakati wa heri, wakati wa mwambo pia,
Mambo yote kuwa shwari, ama kuharibikia,
Wakati wa kunawiri, ama kutanga na njia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Kuna wakati wacheka, siku zingine kulia,
Wakati wa kuridhika, ama mambo kuchachia,
Siku za kukubalika, ama za kukuchukia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Kupata nguvu kusema, ama kusikilizia,
Kunena kwayo hekima, ama bila fikiria,
Kupata yako heshima, kudharaulika pia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Kila utakachopanda, kumbuka kuvuna pia,
Kufanya unalopenda, ama kukuamulia,
Uhuru utakokwenda, ama wakakufungia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Leo wala na kushiba, kesho njaa kuingia,
Ukajaziwa kibaba, ama wakakuibia,
Ukapata mara saba, kuibiwa mara mia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Wakati wa kupokea, ujuwe kutowa pia,
Raha zikikunogea, juwa kuna kujutia,
Leo ukichekelea, kesho shida vumilia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Kuna siku za furaha, na siku zenye udhia,
Kuishi maisha raha, ama shida kuingia,
Ukashukiwa na jaha, ama kusota dunia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Utapata marafiki, kesho watakukimbia,
Utahimili mikiki, ama siku kuumia,
Utaikosa limki, ama kesho kukujia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Tena kuna kuzaliwa, kisha kuna kufa pia,
Kuna karama kupewa, na kushindwa itumia,
Afya njema ikawa, maradhi kukuingia,
Mambo haya hutokea, kila jambo kwa wakati.

Ya kusema nimesema, najua mumesikia,
Nimeipata karama, haya nikawaambia,
Ninagota kaditama, ni lenu kufikiria,
MAMBO HAYA HUTOKEA, KILA JAMBO KWA WAKATI.

Monday, December 8, 2008

Miaka 47: Twaweza kutabasamu?

Awali Bismillah, sifa zake Maulana,
Hii yangu istilahi, nimeifikiri sana,
Siitaki ikirahi, nifikiripo kwa kina,
Twaweza kutabasamu?

Twaweza kutabasamu? pengine ningeuliza,
Kama swali ni gumu, nani atayetujuza?
Nani ni lake jukumu, ukweli kutueleza,
Twaweza kutabasamu?

Hao wenye tamrini, kote wameshatandama,
Wengine waturubuni, maadili yanazama,
Wengine watufitini, twakosa pa kuegama,
Twaweza kutabasamu?

Twasema tupo huru, tena twasherekea,
Ni kweli na haidhuru, lakini tunaumia,
Twapata ufurufuru, ufisadi kuzidia,
Twaweza kutabasamu?

Viongozi wenye nia, tulonao ni wachache,
Wengine watuibia, akili zao macheche,
Nasi tunawaambia, tabia hizo waache,
Twaweza kutabasamu?

Wanaiba tena vyote, wanakuwa wajeuri,
Ili sisi tusipate, ila wao ufahari,
Yaani sisi tusote, ili wao washamiri,
Twaweza kutabasamu?

Uhuru ni kitu gani, labda tungefahamu,
Maisha yetu ni duni, viongozi wadhalimu,
Kufikiri wakunguni, bali wapenda takwimu,
Twaweza kutabasamu?

Kila tukitaradhia, inatubidi kusota,
Lini tunaingojea, maezi yetu kupata?
Wao hujizidishia, ila sisi tunagota,
Twaweza kutabasamu?

Kuhusu hayo madini, twasema kila uchao,
Mikataba wasaini, kujali nafsi zao,
Nchi yawa masikini, huku ukwasi inao,
Twaweza kutabasamu?

Uhuru wa kifikra, twahitaji utumia,
Fikra ziso marara, zenye kutusaidia,
Nchi yetu ikang'ara, ndicho tunategemea,
Twaweza kutabasamu?

Tuudumishe umoja, tuepuke ubaguzi,
Tusingoje siku moja, kwa wabovu viongozi,
Waondoke mara moja, kuwafuga hatuwezi,
Twaweza kutabasamu?

Twataka kutabasamu, twaihitaji sababu,
Sababu tena muhimu, uhuru uwe dhahabu,
Ili sote kwa kaumu, tuuenzi pasi ta'bu,
TWAWEZA KUTABASAMU?

Tuesday, December 2, 2008

Msamaha

Hakuna alokamilika, sote tuna mapungufu,
Hutokea kengeuka, kwani si wakamilifu,
Binadamu hupotoka, huonesha udhaifu,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Usiogope kukosa, sote tumeumbwa hivyo,
Ni mtego tunanasa, vile tufikiriavyo,
Ama tukajenga visa, mengi t'watendeavyo,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Wala sione aibu, kuuomba msamaha,
Mwenye kukosa hutubu, wala si kukosa raha,
Neno zuri ndo wajibu, kwa kuitunza staha,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Samahani neno zuri, kwa wanaotuzunguka,
Tukosapo tukikiri, tunazidi heshimika,
Huo ndiyo ujasiri, tena usio na shaka,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Haifai ujeuri, haifai endekeza,
Ijenge yako nadhari, watu itawapendeza,
Wala siyo jambo zuri, wenzako ukawakwaza,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Makosa hurekebisha, zile tofauti zetu,
Msamaha huboresha, tuishivyo na wenzetu,
Upendo huimarisha, udugu kati ya watu,
Pale unapokosea, basi omba msamaha.

Hakuna aliye mwema, kwa asilimia mia,
Wenzetu wakitusema, haipaswi kuwanunia,
Makosa yanatupima, uwezo kuvumilia,
PALE UNAPOKOSEA, BASI OMBA MSAMAHA.