Thursday, November 27, 2008

Wakati huhukumu

Na waliweza kutudanganya,
Wakatufanya mabwegenyanya,
Wakatufanya tuso maana,
Wakadhani kwa kudanganyana,
Basi watadumu sana!

Na walishasahau ya kwamba,
Ajuaye ni yeye Muumba,
Nini kitakachokuja kesho,
Wakadhani wao so special,
Kumbe nao ni michosho!

Na wakayakwepa majukumu,
Yaliyokuwa na umuhimu,
Wakayafanya yale ya kwao,
Yalokuwa na faida kwao,
Na kwa familia zao!

Na walishazowea vibaya,
Wakadhani sote tu maboya,
Tudanganywe kirahisi sana,
Tusichambue hayo kwa kina,
Wala 'singewezekana!

Na waliambiwa wakabisha,
Kwamba wivu watubabaisha,
Wakaendekeza ufisadi,
Kuzidi kuwa wakaidi,
Tena ni kwa makusudi!

Wakasema tule hata nyasi,
Wao wasafiri kwa ukwasi,
Kufisadi pasi hata wasi,
Wahojio ikawa utesi,
Sababu ya wao ubinafsi!

Na wakati umewahukumu,
Kwa kuitimiza yetu hamu,
Tumewachinjia baharini,
Na kupora tonge mdomoni,
Na wapo mahakamani!

Na wakati nao umesema,
Matendo yao umeyapima,
Na utajulikana ukweli,
Tutoe hukumu sitahili,
Wapate yao halali!

Na wengine nao wajifunze,
Ili tamaa zisiwaponze,
Wajue kwamba tupo makini,
Wasidhani ni kama zamani,
Asilani abadani!

4 comments:

 1. Ahsante sana kwa kunitembelea mara kwa mara. Karibu tena na tena pasi kuchoka.
  Alasiri njema.

  ReplyDelete
 2. hey kazi nzuri, FadhyM. good luck.

  ReplyDelete
 3. Ahsante sana Imani, nakushukuru sana kwa kuzuru kijijini humu. Tafadhali usikose kuzuru tena na tena.
  Karibu sana.

  ReplyDelete