Wednesday, November 19, 2008

Lila na Fila

Hatujui mwalimu wao ni nani,
Hakuwa'mbia haya toka zamani,
Wangekuwa nayo mwao akilini,
Wangemwelewa.

Pengine walitoroka darasani,
Na somo likawapitia pembeni,
Hawajui lolote mwao vichwani,
Tumeingiliwa.

Hawayajui yale ya vitabuni,
Ndiyo maana hawana hata soni,
Ndiyo maana hawanayo imani,
Tumeshavamiwa.

Maneno wayatoayo midomoni,
Huwa yenye kujaa matumaini,
Nasi hudiriki hata kuamini,
Kumbe twaibiwa.

Matendo yao ni kama ukatuni,
Matendo na ahadi havifanani,
Na wao huridhika maofisini,
Tunatawaliwa.

Zamani tulikuwa hatuyaoni,
Tukiyaona twayasemea chini,
Maisha yetu yakazidi uduni,
Hawakuelewa.

Kitu ambacho wao wanatamani,
Kamwe tena asilani abadani,
Tusifunguke mboni zetu machoni,
Tuzidi onewa.

Haiwezekani kamwe haiwezekani,
Hatutonyamazia kama zamani,
Kwani hila zao tumezibaini,
Tumewaelewa.

Uongo na kweli hautangamani,
Hata utumie gundi ya dukani,
Hatutachoka kusema asilani,
Hatutaonewa.

Tunawataka mtuelewe!

1 comment:

  1. Saluti mkuu!
    Nakupa heshima zote kwa shairi lako la lila na fila. Umeonesha ukomavu mkubwa katika tasnia ya ushairi. Ni maneno machache, lakini yamebeba ujumbe mkubwa sana. Kwa wale wenye kufikiri kwa makini. Lakini tatizo tulilonalo watawala huwa hawana muda wa kuyasoma haya. Pia shairi la taifa ni mwalimu, ni amali katika jamii yetu.
    Kaza buti bwa'mdogo, waambie, hata wakiweka pamba ipo siku zitatoka na watayasikia tu maneno haya.
    Keep it up.

    ReplyDelete