Sunday, November 30, 2008

Hao watu

Walipewa madaraka,
Tena wakakubalika,
Pia wakaheshimika,
Nasi tukawatambua.

Madaraka yakazidi,
Yakazaa makusudi,
Ikazaa ukaidi,
Kiburi kuwaingia.

Wa kuonya wakaonya,
Na wao wakawasonya,
Wakazidi tudanganya,
Tukabaki twaumia.

Wakasema tule nyasi,
Tena bila wasiwasi,
Kwa kiburi cha kibosi,
Wao wakatuambia.

Nasi tungefanya nini?
Waliushika mpini,
Watu wa madarakani,
Jeuri 'liwasumbua.

Muda nao ukaenda,
Hakikupona kidonda,
Tulijua tutashinda,
Na sasa inatokea.

Twawakumbusha wenzetu,
Wasipungukiwe utu,
Vyeo siyo malikitu,
Mwisho wake hufikia.

Muda ndiyo huongea,
Muda hautobagua,
Nani 'tayeuzuia?
HAKUNA NINAKWAMBIA.

5 comments:

 1. Shairi lako limeshiba.

  ReplyDelete
 2. men, this one is deep! keep it up brother!

  ReplyDelete
 3. Ahsante sana. Ntajitahidi kukaza buti.
  Karibu tena na tena.

  ReplyDelete
 4. Nakuonea wivu kwani najaribu kuandika au niseme napenda kuandika mashairi ila... kazi nzuri sana usiache

  ReplyDelete
 5. Ila nini?
  Wala usijali dadaangu. Ukishindwa kuandika wewe ntaandika mimi, wewe utayasoma kisha utashusha pumzi.
  Nakushukuru sana da Yasinta kwa kunikumbuka mara kwa mara.
  Karibu tena.
  Pia kazi njema.

  ReplyDelete