Sunday, November 30, 2008

Hao watu

Walipewa madaraka,
Tena wakakubalika,
Pia wakaheshimika,
Nasi tukawatambua.

Madaraka yakazidi,
Yakazaa makusudi,
Ikazaa ukaidi,
Kiburi kuwaingia.

Wa kuonya wakaonya,
Na wao wakawasonya,
Wakazidi tudanganya,
Tukabaki twaumia.

Wakasema tule nyasi,
Tena bila wasiwasi,
Kwa kiburi cha kibosi,
Wao wakatuambia.

Nasi tungefanya nini?
Waliushika mpini,
Watu wa madarakani,
Jeuri 'liwasumbua.

Muda nao ukaenda,
Hakikupona kidonda,
Tulijua tutashinda,
Na sasa inatokea.

Twawakumbusha wenzetu,
Wasipungukiwe utu,
Vyeo siyo malikitu,
Mwisho wake hufikia.

Muda ndiyo huongea,
Muda hautobagua,
Nani 'tayeuzuia?
HAKUNA NINAKWAMBIA.

Thursday, November 27, 2008

Wakati huhukumu

Na waliweza kutudanganya,
Wakatufanya mabwegenyanya,
Wakatufanya tuso maana,
Wakadhani kwa kudanganyana,
Basi watadumu sana!

Na walishasahau ya kwamba,
Ajuaye ni yeye Muumba,
Nini kitakachokuja kesho,
Wakadhani wao so special,
Kumbe nao ni michosho!

Na wakayakwepa majukumu,
Yaliyokuwa na umuhimu,
Wakayafanya yale ya kwao,
Yalokuwa na faida kwao,
Na kwa familia zao!

Na walishazowea vibaya,
Wakadhani sote tu maboya,
Tudanganywe kirahisi sana,
Tusichambue hayo kwa kina,
Wala 'singewezekana!

Na waliambiwa wakabisha,
Kwamba wivu watubabaisha,
Wakaendekeza ufisadi,
Kuzidi kuwa wakaidi,
Tena ni kwa makusudi!

Wakasema tule hata nyasi,
Wao wasafiri kwa ukwasi,
Kufisadi pasi hata wasi,
Wahojio ikawa utesi,
Sababu ya wao ubinafsi!

Na wakati umewahukumu,
Kwa kuitimiza yetu hamu,
Tumewachinjia baharini,
Na kupora tonge mdomoni,
Na wapo mahakamani!

Na wakati nao umesema,
Matendo yao umeyapima,
Na utajulikana ukweli,
Tutoe hukumu sitahili,
Wapate yao halali!

Na wengine nao wajifunze,
Ili tamaa zisiwaponze,
Wajue kwamba tupo makini,
Wasidhani ni kama zamani,
Asilani abadani!

Tuesday, November 25, 2008

Siku Moja

Kwa hakika ipo inakuja,
Hatuhitaji tena kungoja,
Hatutazisikiliza hoja,
Tutasimama sote pamoja,
Tukiwa na nia yetu moja.

Sauti zetu zitasikika,
Kote zinakoweza kufika,
Ili wafahamu tumechoka,
Kuendelea kunyanyasika,
Ipo inakuja kwa hakika.

Tutadhihirisha yetu nguvu,
Ya hoja na siyo ya mabavu,
Kwa watufanyao wapumbavu,
Watalikalia kuti kavu,
Katika siku hiyo angavu.

Ni vema tukayasema haya,
Kwa uwazi pasipo kugwaya,
Kwa karatasi ama kwa waya,
Tukasikika kwa kila kaya,
Ili mambo yasiye mabaya.

Tunataka 'wao' wafahamu,
Sisi hatunayo tena hamu,
Twachoshwa na wao udhalimu,
Ambao kwetu ni kama sumu,
Isiyotufaa wanadamu.

Wamekula sana vya kutosha,
Na hawakutaka kubakisha,
Hawataki kujirekebisha,
Hawajui muda unakwisha,
Nani atakayewakumbusha?

Wamenogewa hawashituki,
Hawaumizwi na yetu dhiki,
Huja nazo ahadi lukuki,
Ingawa hazitekelezeki,
Hutushawishi kuzisadiki.

Wanafikiri hatutoweza,
Walipo 'wao' kuwafukuza,
Mizizi yao wameshikiza,
Wengine na kwa nguvu za giza,
Siku yaja 'wao' kuteleza.

Nakutaka nawe usikie,
Ili wengine uwaambie,
Inatupasa tudhamirie,
Haraka siku tuifikie,
Kwani tumechoka sana sie.

Tukakusanyane sisi sote,
Asibakie mtu yeyote,
Huku na kule na kote kote,
Taarifa hizi wazipate,
Wale yamini na wasisite.

Lini siku hiyo itafika?
Kama siyo leo kwa hakika?
Ni nani ambaye hatofika?
Huyo asemaye karidhika,
Na ole wake tukimshika.

Siku moja wala siyo mbili,
Hatufichi twasema ukweli.

Sunday, November 23, 2008

Hao hao

Wameyafaidi matunda,
Hawakuwekewa mizengwe,
Mbona walikula kwa raha
Na bado wanatafuna tu!
Hao wamefanya hivyo
Tangia tangu na tangu.

Wengine huwa hawapendi
Hata siku moja,
Kuwaona wa nje ya mnyororo,
Akionja
Japo tone la mchuzi,
Akinawa
Walau mikono yake.

Hawapendi kamwe iwe hivyo.
Wamehalalisha ubaguzi,
Unaotokana na mfumo,
Wao ulio mbaya.
Mfumo mbovu mno
Wenye utenganifu,
Sababu wao,
Wanacho kila kitu.

Na hawa,
Hawana japo thumni.

Walikula wao ile keki,
Sasa hawawataki na wengine,
Nao waile.
Wameimaliza chai yote,
Sasa wanataka kuikung'uta
Hata chupa ya chai.

Wamekomba mboga yote
Sasa wanauramba hata mwiko.
Walionja asali,
Hawajauchonga mzinga
Bali wameukombeleza,
Wote kabisa!

Ni kweli
Waliyaweza tangu jana,
Hata leo wameweza,
Lakini wanaisahau
Adhabu ya muda.
Kwamba hata wasipotaka,
Muda utafika tu.

Watoto wa masikini,
Watasoma tu!

Muda huo ni lini?
Ni huu tulionao.

Saturday, November 22, 2008

Wakati

Sema neno usemale, yangu mie sikiale,
Fanya mambo ufanyale, siige ya mtu yule,
Cha mtu mavi usile, kamwe usikigusile,
Wakati ndiyo mwamuzi, huwezi pingana nao.

Sijisahau kivile, kuwa muda waendale,
Usidhani ni milele, tabaki na cheo kile,
Sishindwe hata simile, cheo siking'ang'anile,
Wakati ndiyo mwamuzi, huwezi pingana nao.

Wautaka utotole, ni kipi ukifanyile,
Wakati huwa kichele, waenda mwendo mwendole,
Wala hauachi chule, kusema waonale,
Wakati ndiyo mwamuzi, huwezi pingana nao.

Wakati siyo jefule, na haugongi kengele,
Kutoa ishara ile, mwendo wa kifukulile,
Siufanye mgolole, kuupenda mvaole,
Wakati ndiyo mwamuzi, huwezi pingana nao.

Siwe kama duduvule, kutamani kasimile,
Kishafikia kilele, waachie watu wale,
Siutibie mkole, wakati siende mbele,
Wakati ndiyo mwamuzi, huwezi pingana nao.

Wakati kama mtale, kizubaa wakatale,
Tumia utumiale, sichekwe na watu wale,
Haunaye mteule, umpendelee yule,
Wakati ndiyo mwamuzi, huwezi pingana nao.

Jiepushie utule, pamoja na hiyo ndwele,
Fanya kama mtungule, jambo lile muda ule,
Sijisahau kwa vile, wakati haurudile,
Wakati ndiyo mwamuzi, huwezi pingana nao.

Ukisema wasemale, wakati huupingile,
Kibisha taumiale, takutupa mkonole,
Sasa sipowezale, silaumu mtu yule,
WAKATI NDIYO MWAMUZI, HUWEZI PINGANA NAO.

Wednesday, November 19, 2008

Lila na Fila

Hatujui mwalimu wao ni nani,
Hakuwa'mbia haya toka zamani,
Wangekuwa nayo mwao akilini,
Wangemwelewa.

Pengine walitoroka darasani,
Na somo likawapitia pembeni,
Hawajui lolote mwao vichwani,
Tumeingiliwa.

Hawayajui yale ya vitabuni,
Ndiyo maana hawana hata soni,
Ndiyo maana hawanayo imani,
Tumeshavamiwa.

Maneno wayatoayo midomoni,
Huwa yenye kujaa matumaini,
Nasi hudiriki hata kuamini,
Kumbe twaibiwa.

Matendo yao ni kama ukatuni,
Matendo na ahadi havifanani,
Na wao huridhika maofisini,
Tunatawaliwa.

Zamani tulikuwa hatuyaoni,
Tukiyaona twayasemea chini,
Maisha yetu yakazidi uduni,
Hawakuelewa.

Kitu ambacho wao wanatamani,
Kamwe tena asilani abadani,
Tusifunguke mboni zetu machoni,
Tuzidi onewa.

Haiwezekani kamwe haiwezekani,
Hatutonyamazia kama zamani,
Kwani hila zao tumezibaini,
Tumewaelewa.

Uongo na kweli hautangamani,
Hata utumie gundi ya dukani,
Hatutachoka kusema asilani,
Hatutaonewa.

Tunawataka mtuelewe!

Taifa ni Mwalimu

Wote huamini hivyo,
wenye kiburi hubisha,
kwa jeuri ya vyeo vyao,
kwa jeuri ya elimu zao.

Waseme maneno gani?
hawajui li dhahiri kwao,
wamechoka kufikiri,
wamechoka kabisa.
Busara i wapi?

Wote hupitia kwake,
yeye alojaa wito wa kweli,
kwa kazi yake.
Wameyasahau hayo,
aki ya Ngai!

Busara zote hutoka kwake,
tena huzipika kwa ustadi mkubwa,
hakuna ampitaye maarifa,
yu mpishi alobobea.
Hawafahamu hilo.

Ustawi wa maarifa yao,
watawala wakuu hawa,
wa ulimwengu wote,
umetoka kwake.
Abishae maneno haya,
na aseme kwa thabiti.

Dunia haina shukrani hata,
hapana,
si dunia tena,
bali ni wanadunia hawa,
siyo hawa,
bali ni sisi.

Na wao wenye nazo,
hizo mamlaka.

Hujisahaulisha,
kwa makusudi kabisa,
huona si halali wao kupewa,
hizo stahili stahiki.

Bila wao,
ningewakumbusha,
hakuna tena taifa,
litakuwepo vipi?
katikati ya umbumbumbu?