Sunday, April 6, 2008

ni kitu gani?

Nakuleteeni swali, wajuzi wa maarifa,
Mlojaliwa akili, na bongo zisizokufa,
Muwezao ona mbali, naombeni maarifa,
Mapenzi ni kitu gani?

Mapenzi ni kitu gani, swali langu nauliza,
Kwani yalianza lini, hadi leo yatatiza,
Watu kuzama dimbwini, mbona yanawaumiza,
Mapenzi ni kitu gani?

Ama kuna tofauti, na yale ya vitabuni,
Yetu kizungumkuti, wengi wayalaani,
Kwamba raha hawapati, tena humo mapenzini,
Mapenzi ni kitu gani?

Niliyaanza zamani, nami pia nikapenda,
Tena niliyaamini, nazo siku zikaenda,
Pamoja nayo imani, mpenzi akanitenda,
Mapenzi ni kitu gani?

Walisema kupotea, ndiko kuijua njia,
Kidogo nikatulia, maumivu kupungua,
Ni kweli niliumia, nikawaza mara mia,
Mapenzi ni kitu gani?

Ikajatokea tena, mapenzini nikazama,
Wengine sikuwaona, kwake moyo kutuwama,
Nilimpenda kwa sana, sikujali wakisema,
Mapenzi ni kitu gani?

Ikajatokea naye, kanifanya kuumia,
Yule nimwaminiaye, ubaya kunifanyia,
Nani sasa awezaye, swali akanijibia,
Mapenzi ni kitu gani?

Huyu mwingine wa tatu, alinikata maini,
Pengine hanao utu, kashindwa kunithamini,
Kaona si malikitu, sipati jibu moyoni,
Mapenzi ni kitu gani?

Kapasi kwenda chuoni, nikabaki mtaani,
Hesabu zake kichwani, zikagoma abadani,
Akaniona wa nini, basi kanipiga chini,
Mapenzi ni kitu gani?
Huyu kaenda Ulaya, akasema sasa basi,
Kaniumiza vibaya, sitolipiza kisasi,
Sikumfanyia baya, akaninyima nafasi,
Mapenzi ni kitu gani?

Na huyu ile zawadi, kampa mtu mwingine,
Akaivunja ahadi, kwa kuzaa na mwingine,
Nadhani ni makusudi, sijiulizi jingine,
Mapenzi ni kitu gani?

Nikaipata adhabu, mapenzi yakanitesa,
Zingenipanda ghadhabu, dali wangu kumkosa,
Sijapata bado jibu, ndani kuna nini hasa,
Mapenzi ni kitu gani?

Wanasema yana raha, mi’ raha sijaipata,
Wanasema ni furaha, machozi yangenifuta,
Na kama siyo karaha, mbona mie nimesota,
Mapenzi ni kitu gani?

Ya kutoka kwa mzazi, hakika nayaamini,
Lakini ya kwa mpenzi, nimeona walakini,
Nishafanyiwa ushenzi, nikazama majonzini,
Mapenzi ni kitu gani?

Mapenzi ni raha gani, mbona wayasifia,
Ama yamo nchi gani, watu wasikoumia,
Hebu jifikirisheni, majibu kunipatia,
Mapenzi ni kitu gani?

Nawauliza malenga, nami nitoke kizani,
Haya watu wanalonga, kweli yapo duniani?
Ama kunayo machanga, yaso na ladha kwa ndani?
Mapenzi ni kitu gani?

Kwani huwa vipivipi, hayo mapenzi ya kweli?
Washayaonja wangapi, leo waseme ukweli,
Tena siyo ya makapi, yaso na ubaradhuli,
Mapenzi ni kitu gani?

Semeni semeni jama, nahitaji kuelewa,
Naogopa kuja zama, vile nilivyotokewa,
Nifahamu kuyapima, nisipate kuchachawa,
Mapenzi ni kitu gani?
Swali nimewauliza.