Monday, September 17, 2007

kama wao!

niwaonapo nawaza kitu kichwani,
lakini nashindwa kujua nitafanyaje,
niwaonapo ni kama naona kivingine,
wala siyo vile ningestahili mimi,
na sijui wao wanajisikiaje,
wanapokuwa kama wao.

Wao hawakutaka kuwa kama sisi,
Ila walitaka sisi tufuate kama wao,
Na mavazi wayaletayo kwetu,
Hutufanya tuige ili nasi pengine tuwe,
Kama wao.

Rangi yetu wanaifahamu tangu mapema,
Pale walipokuja kwa mara ya kwanza,
Lakini wakaona kama haifai,
Wakaamua kutuonesha huruma yao,
Wakatuletea madawa mazuri sana,
Ili dada zetu wayatumiapo mwilini,
Rangi zao ziweze kubadilika,
Ziwe zenye kung’aa kama wao.

Walitukuta tunaabudu kivyetuvyetu,
Tena imani zetu zilikuwa na nguvu sana,
Wakakusudia kutudhoofisha kiimani,
Wakazileta zao walizosema ndizo bora,
Na kwamba zetu zilikuwa ni ushenzi mtupu,
Nasi tukazipokea kwa mkono yote,
Ili nasi tuabudu kama wao.

Wakavuruga mtindo wa utawala wetu,
Uliokuwa bora sana kushinda wa kwao,
Wakalazimisha kututawala wao,
Na hata waliposhindwa na kuondoka,
Wakawa wametuachia mfumo wao,
Nasi tukaona ni fahari sana,
Kuwa na mfumo kama wao.

Utamaduni wetu ulikuwa ni ushenzi kwao,
Wakaleta muziki wa kwao wao,
Kwa kuwa tushaathirika vichwani mwetu,
Tuaona ndicho kitu kitufaacho zaidi,
Tukautupa wa kwetu tukaukumbatia wa kwao,
Hata sasa bado tuna ugonjwa ule,
Hata muziki bado tunaupenda ule ule,
Maana tunapenda tuonekane kama wao.

Kila kitu cha kwetu twaona hakifai,
Tumemezwa na mbaya kasumba,
Na inatutafuna kwani hatutaki kubadilika,
Twavidharau vyetu na kukumbatia vyao,
Hata lugha yetu haifai,
Tuongeapo twachanganya maneno,
Kama siyo kuongea yao kabisa,
Ili hata wenzetu watuogope,
Tunapenda tuonekane kama wao.

1 comment:

  1. This comment has been removed by a blog administrator.

    ReplyDelete