Tuesday, August 7, 2007

wamepata wapi?

Wamejenga matabaka, tawala na tawaliwa,
Wameivuka mipaka, nchi yazidi kuliwa,
Wao hawanayo shaka, maana wamenogewa,
Wamepata wapi, huo ujasiri,
Kama si kwa kura zetu?

Maisha yawa magumu, magumu kupindukia,
Twapaa kwenda kuzimu, kusikokuwa na njia,
Wao washika hatamu, raha zimewanogea,
Wamepata wapi, huo ujasiri,
Kama si kwa kura zetu?

Kwao yawaka neema, kwingine umasikini,
Mwenye macho atazama, aiona khali duni,
Uchumi wazidi zama, wazama chini shimoni,
Wamepata wapi, huo ujasiri,
Kama si kwa kura zetu?

Wao walitowa khanga, kipindi cha kampeni,
Kauli mbiu tunga, maujumbe kusheheni,
Vitini walipotinga, ahadi tupwa kapuni,
Jiulize,
Wamepata wapi, huo ujasiri,
Kama si kwa kura zetu?

Walisemea madini, tena walisema sana,
Wakatowa tumaini, kwamba mambo yangefana,
Ingetupwa makapuni, mikataba ka’ ya jana,
Wamepata wapi, huo ujasiri,
Kama si kwa kura zetu,

Ni kwa hizo kura zetu, wamekipata kiburi,
Huu umasikini wetu, wao hauwaathiri,
Hawapo baina yetu, kwao maisha mazuri,
Wamepata wapi, huo ujasiri,
Kama si kwa kura zetu?

Tuliwapa wao kura, tukawanyima wengine,
Kupata maisha bora, tuwaze njia nyingine,
Hali yetu yadorora, si kama siku zingine,
Wamepata wapi, huo ujasiri,
Kama si kwa kura zetu?

Ni kura zetu wenyewe, nadhani tulikosea,
Kutaka tufanikiwe, kosa kutolirudia,
Yatubidi tuelewe, wenzetu hawana nia,
Tujiulize,
Wamepata wapi, huo ujasiri,
Kama si kwa kura zetu?

No comments:

Post a Comment