Monday, July 2, 2007

Sala ya Mtawala.

Ee Mwenyezi Mungu,
Baba wa rehema,
Uliyeiumba mbingu na dunia,
Uliyeliweka tabaka la watawala,
Pia ukaweka tabaka la watawaliwa,
Wastahili sifa zote.

Ee Mwenyezi Mungu,
Kwani mamlaka zote zatoka kwako,
Umewaagiza wananchi kuzitii,
Nao watazitii daima.

Ee Mwenyezi Mungu,
Ahsante sana kwa kunichagua mimi,
Kuwa mtawala wa viumbe hawa,
Kwa kuwa ninastahili sana,
Kama ambavyo umeona wewe,
Hakuna mwingine kama mimi.

Ee Mwenyezi Mungu,
Ninakushukuru kwa kunipa ujasiri,
Wa kuweza kuwatawala watu wako,
Hata katika vipindi vigumu mno,
Bado ninasimama imara kabisa,
Hakika ninakushukuru.

Ee Mwenyezi Mungu,
Sina budi kutowa shukurani zangu,
Kwa kunipa uso mkavu kabisa,
Wakati mwingine tabasamu la bashasha,
Nisimamapo ma kuudanganya umma,
Hata katika mambo yaliyo dhahiri,
Ninasema ahsante sana.

Ee Mwenyezi Mungu,
Nipe ujasiri zaidi niviruke viunzi,
Na kuwaangamiza maadui wangu,
Unifanye shupavu kama mfalme Daudi,
Niweze kuwaangamiza wapinzani wangu,
Ili niwe na hakika ya kutawala,
Milele na milele.

Ee Mwenyezi Mungu,
Ee Yehova Yire, Mungu wa Israel,
Izidishie neema familia yangu,
Ifaidike vema na utajiri wa nchi hii,
Ambayo wewe umetuchagua tuifaidi.

Ee Mwenyezi Mungu,
Uniondolee huruma moyoni,
Pale inaponibidi kuyatanguliza maslahi yangu,
Lakini unijalie sura ya unyenyekevu,
Hata kama moyoni haitomaanisha hivyo,
Ili wananchi waizidishe imani yao kwangu.

Ee Mwenyezi Mungu,
Ninakuomba ukibariki kinywa changu,
Kiweze kuyatoa maneno matamu mithili ya asali,
Na uwafanye wananchi wazidi kuwa wadanganyika,
Ili utawala wangu udumu daima dawamu,
Na usifutike katika vitabu,
Vya historia.

Ee Mwenyezi Mungu,
Ninasema ahsante sana,
Kwani ulisema utanifanya kichwa daima,
Basi katika hayo yote,
Ninaomba na kushukuru,
Nikisema,
Amina.

2 comments:

  1. Oi, achei teu blog pelo google tá bem interessante gostei desse post. Quando der dá uma passada pelo meu blog, é sobre camisetas personalizadas, mostra passo a passo como criar uma camiseta personalizada bem maneira. Até mais.

    ReplyDelete
  2. dogo keep it up wachambue na viongozi wetu sio wanaenda nje tu waige na mifano ya nchi za wenzetu hasa ktk kitengo cha miundo mbinu mfano barabara.na mambo ya rushwa ufisadi tunaumia watu wa chini.poa best.

    ReplyDelete