Sunday, July 1, 2007

Hotuba ya Mtawala.

Ndugu wananchi,
Ninazitowa shukrani zangu,
Tena shukurani za dhati,
Kwa kunionesha imani kubwa,
Mliyoanyo kwangu mimi,
Hata mkanichagua.

Ndugu wananchi,
Si kwamba ninastahili sana,
Kuliko mtu mwinginewe,
Bali nimejitowa kuwa mtumishi,
Mtumishi wenu mwadilifu,
Nakuombeni ushirikiano.

Ndugu wananchi,
Kuna matatizo ya msingi,
Pamwe wale maadui watatu,
Yaani umasikini, ujinga na maradhi,
Na sasa kaka yao rushwa,
Tutasimama imara kwa pamoja,
Na kuyatokomeza.

Ndugu wananchi,
Tutahakikisha maji yanapatikana,
Tena yaliyo safi na salama,
Pia huduma za afya kwa wananchi,
Zitatolewa kwa moyo mmoja,
Nayo malaria itatokomezwa kabisa.

Ndugu wananchi,
Ukimwi utabakia historia,
Elimu ya uhakika itatolewa,
Na mitaji ya kutosha ya ujasiriamali,
Ili tuondokane nao hata ukahaba,
Tukiushinda umasikini.

Ndugu wananchi,
Miundombinu itaboreshwa,
Ili muweze kusafiri hata kwa teksi,
Mahala popote nchini humu,
Umeme nao utakuwa wa uhakika,
Hakutakuwa na mgao wala giza tena,
Yaani kutakuwa Ulaya Ulaya.

Ndugu wananchi,
Tutajenga mashule na mavyuo,
Na kukiboresha kiwango cha elimu yetu,
Hata wapiga debe watakuwa ni wasomi,
Na tutaongeza tija.

Ndugu wananchi,
Tunayo mengi ya kuyajadili,
Lakini kwanza tukafanye kazi,
Tushikamane kwa nguvu moja,
“Mshikamano daima, mbele daima”,
Mungu ataibariki nchi yetu.

Ahsanteni kwa kunisikiliza!

No comments:

Post a Comment