Friday, June 15, 2007

ziwapo butu

Si kwa makali,
Nini kingekatwa nayo?
Hudhani ni vigumu,
Waonapo siyo rahisi,
Itawezekana vipi?
Haitowezekana bwana!

Si rahisi kiasi hicho,
Kama wanavyofikiria,
Si rahisi hata kidogo,
Inahitajika nguvu,
Tena nguvu ya ziada.

Wala si vigumu kabisa,
Wao ndiyo wanadhani,
Kwamba ni vigumu,
Hata siku moja,
Haiwezi kuwa hivyo.

Wanahitaji msaada sana,
Wao wenye uvivu,
Wa kufanya tafakuri,
Tena zenye kina,
Ni wavivu ati!
Kweli eeh?

Wanaamini hivyo,
Kwamba wanaweza sana,
Kuzififisha kabisa,
Bongo zenye kuthubutu,
Zisizo lala kamwe,
Daima zilizo vitani.

Wanazifanya ziwe butu,
Zisiweze asilani abadani!
Kutufanya tuwe imara,
Na kamwe hawatopenda,
Hawatopenda asilani.

Nguvu yetu i dhahiri,
Yenye kuonesha vema,
Dhamira zetu za dhati,
Kupingana nao,
Pasipo maslahi yetu,
Penye dhulma ilokithiri.

Yenye kuufuata upepo,
Ni ile bendera,
Hatufanani nayo hata!
Tu na msimamo wetu.

Hawatousimamisha,
Hawatousimamisha kamwe,
Muda, muda utafika tu,
Utawahukumu wao,
Kwa kuwa siku itafika tu,
Ndiyo, siku haitofika,
Wala,
Haipo mbali.

Watake wasitake wao,
Siku ya panga butu,
Litakapoyaonesha yake makali,
Litakata bila huruma,
Twalinoa vema, twalinoa hasa,
Twalinoa vema, twalinoa sasa,
Ndiyo!
Ndiyo, ndiyo siku itafika.

No comments:

Post a Comment