Saturday, June 9, 2007

wangu rafiki!

Nuru ya jua uamkapo,
Tumaini zaidi liwepo,
Na huzuni ikuondokapo,
Pindi moyo ufarijikapo,
Farijika nami.

Usilemewe sana kichwani,
Moyo siutose majonzini,
Walishasema hapo zamani,
Basi jipe amani moyoni,
Ufurahi nami.

Muda ungeweza rudi tena,
Tungeipenda siku ya jana,
Idumu muda mrefu sana,
Hakika tungefurahiana,
Jiliwaze nami.

Safari ndiyo yetu maisha,
Mwingine yake kakamilisha,
Kipande tulichokibakisha,
Nasi siku moja kitakwisha,
Jiliwaze nami.

Pengo lake huleta majonzi,
Moyo ukajawa na simanzi,
Tukimpa imani Mwenyezi,
Kuwa peke yetu hatuwezi,
Ufurahi nami.

Yahimili hayo maumivu,
Uzidishe ustahimilivu,
Kwa maana Mungu yu na nguvu,
Kuyafanya maisha angavu,
Farijika nami.

Nimetuma maalumu kwa rafiki yangu wa siku nyingi Elminah P. Kessy kwa kuondokewa na mzazi wake. Mungu ampe faraja rafiki yangu, na kuilaza roho ya marehemu mahali pema peponi. Amen.

2 comments:

 1. Asante kwa kutushirikisha kwenye fikra zako. Shairi hilo hapo chini la Kule Nako nimelipenda mno.

  ReplyDelete
 2. nakushukuru sana Ndesanjo kwa kutembelea blog yangu na kuacha maoni hapo. Sina budi kuitumia nafasi hii kukushukuru sana kwa hamasa uliyonitia kwa muda mrefu kuhusu kuanzisha blog. Nimekuwa mfuatiliaji wa Gumzo la Wiki katika gazeti la Mwananchi Jumapili na nimejifunza mengi sana kwako.
  nawaomba na watu wengine wafanye hivyo, ili tuwe na mahala pengi pa kuyasemea yale ambayo tungependa watu wengine wafahamu.
  nakubali kwamba sasa wananchi tunapata mwamko mkubwa sana. tunahitaji juhudi zaidi na zaidi ili tufanye kitu fulani.
  nakukaribisheni nyote katika kijiji changu.
  nakuahidini kuendelea kujitahidi kukupakulieni mashairi mengi kadri ya uwezo wangu.
  tupo pamoja.

  ReplyDelete