Thursday, June 21, 2007

kwani uongo?

Siku moja itafika,
Ninasema kwa hakika,
Siku, siku itafika,
Tutasema tumechoka,
Hata nao vibaraka,
Hakika watateseka.

Siku moja ninasema,
Fungua macho tazama,
Wala usibaki nyuma,
Kwa pamoja kujituma,
Itakuwa siku njema,
Kwa wenye mapenzi mema.

Washatudharau sana,
Kwamba hatuna maana,
Wametufanya watwana,
Thamani yetu hakuna,
Huku wao wajichana,
Mifuko yao kutuna.

Tuling’oa ukoloni,
Tukidhani tumewini,
Kumbe tunao nguoni,
Adui nambari wani,
Waso huruma myoyoni,
Kwa wetu umasikini.

Kila kitu wanauza,
Hakuna wanachosaza,
Ni dhambi kuwauliza,
Uchumi ‘napouchakaza,
Ipo siku tutaweza,
Nasi kuwateketeza.

Nchi ni ya kwetu sote,
Hatukupewa tusote,
Ili wachache wapate,
Na wanyonge tuufyate,
Haikwandikwa tusote,
Haikwandikwa wapate.

Dini ya uwekezaji,
Waja umasikinishaji,
Zao ukandamizaji,
Na kupoteza mitaji,
Wao utajirikaji,
Na marufuku kuhoji!

Siku moja inakuja,
Hatuhitaji kungoja,
Sie sote kwa pamoja,
Tutaikata mirija,
Watabaki kubwabwaja,
Kwa ubwana ulochuja.

Siku hiyo imefika,
Tunapaswa kuamka,
Na kusema tumechoka,
Na kwa kweli watang’oka,
Kwa mizizi waloweka,
Ni kweli tumechoka.

No comments:

Post a Comment