Tuesday, June 5, 2007

duniani humu

Siyo wote wema, ninasema,
Kwa wenye hekima, watapima,
Heri kutazama, ona kama,
Wanayo huruma,
Duniani humu.

Wengine mahiri, kufikiri,
Kisha mashuhuri, kubashiri,
Kutowa vizuri, mahubiri,
Kumbe ni washari,
Duniani humu.

Wengine nuksi, ni waasi,
Wana ibilisi, wa kisasi,
Tamaa ya fisi, wanaghasi,
Siwape nafasi,
Duniani humu.

Kuna marafiki, wanafiki,
Sipopata dhiki, wana chuki,
Watakupa siki, hawataki,
Pate japo laki,
Duniani humu.

Wanaichukia, yako njia,
Watakuzushia,’taumia,
‘Takuharibia, yako nia,
Pate didimia,
Duniani humu.

Ndugu mia tatu, siyo kitu,
Pengine si watu, roho kutu,
Mioyo i butu, sema katu,
Sikupe ufyatu,
Duniani humu.

Ndani ya mapenzi, ni kitanzi,
Mejaa ushenzi, kuna kazi,
Tapata simanzi, moyo ganzi,
Bado hujifunzi,
Duniani humu.

1 comment:

  1. duniani humu!
    kweli kabisa duniani humu ndivyo kulivyo.

    ReplyDelete