Wednesday, June 27, 2007

Buriani Amina Chifupa!

Nasikia radioni, Amina hayupo tena,
Ninashindwa kuamini, umetutoka Amina,
Amina wetu jamani, Amina wetu Amina,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Mola wetu tusikie, twaja kwako Maulana,
Amina tumlilie, mbunge wetu vijana,
Faraja utupatie, usiku hata mchana,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina mbunge wetu, tuliyekupenda sana,
Uliyeonesha utu, kwa wazee na vijana,
Uliyekuwa mwenzetu, tena bila ya hiyana,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina ulitujali, tukakupenda kwa sana,
Juhudi zako za kweli, zilikubalika sana,
Mola wetu mfadhili, lini tutamwona tena?
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Umetuacha jamani, twakulilia Amina,
Ni vigumu kuamini, kuwa hatukwoni tena,
Majonzi yetu moyoni, mbona ni makubwa sana,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Twashindwa kuelezea, jinsi inavyotuuma,
Ni vigumu kuzowea, kupoteza kitu chema,
Wewe ulijitolea, ukweli ukausema,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina bado kijana, umetuacha mapema,
Ndoto zako nyingi sana, ukaamua kusoma,
Kwa marefu na mapana, uiongeze hekima,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina muongeaji, waongea kwa hekima,
Wewe mshereheshaji, Amina ukawa mama,
Amina mpiganaji, vita sasa waitema,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina tulikupenda, ukawa rafiki mwema,
Ona sasa umekwenda, kwa heri hujaisema,
Mauti yamekutenda, basi uende salama,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Pole wanafamilia, pole Tanzania nzima,
Sote tunakulilia, utakumbukwa daima,
Wewe umetangulia, nasi twaja tuko nyuma,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Mola akupumzishe, peponi mahala pema,
Nasi tukajikumbushe, dunia siyo salama,
Mola wetu tuepushe, na hicho chako kiyama,
MOLA UMLAZE PEMA, RAFIKI YETU AMINA.

Ni vigumu kuamini, lakini duniani sisi sote tunapita. Ametangulia mwenzetu. Tunamuomba Mola ailaze roho yake mahali pema peponi. Amen.

1 comment:

  1. hi fadhi we are tired of this poem so please can you prepare another poems,please deal with our leader maovu wanayoyafanya wananchi tunateseka shwanga mwana tutakulinda.do it keep it up

    ReplyDelete