Thursday, June 14, 2007

bongoland

Bongoland ndo nyumbani, unaishi kwa akili,
Tunaishi kimjini, kumejaa utapeli,
Wakuu nao kundini, kupora rasilimali,
Hii ndiyo Bongo.

Bongoland ndo nyumbani, nchi bado i fukara,
Hakuna matumaini, zimeshindwa zao sera,
Twazidi kushuka chini, uchumi siyo imara,
Hii ndiyo Bongo.

Bongoland ndo nyumbani, viongozi si wawazi,
Japo kwenye kampeni, wamwaga hata machozi,
Kututaka tuamini, watafanya vema kazi,
Hii ndiyo Bongo.

Bongoland ndo nyumbani, daima makongamano,
Kofia nzuri vichwani, ujumbe wa mikutano,
Kumbe mwao mioyoni, wawazia pesa nono,
Hii ndiyo Bongo.

Bongoland ndo nyumbani, kufikiri tu wavivu,
Tuhojipo ni kwa nini, twaambiwa tuna wivu,
Si yetu tena madini, twabaki lamba pakavu,
Hii ndiyo Bongo.

Bongoland ndo nyumbani, rushwa sasa takrima,
Unipe kiti bungeni, utalipwa wako wema,
Bado tupo safarini, yetu ya kurudi nyuma,
Hii ndiyo Bongo.

Bongoland ndo nyumbani, ni mibovu mikataba,
Mafuta hadi madini, kwa midogo mirahaba,
Na huko serikalini, pesa nyingi wanaiba,
Hii ndiyo Bongo.

No comments:

Post a Comment