Tuesday, June 5, 2007

akili zao!

Kwa maana hawapendi kuona,
Ukitabasamu japo kidogo kwa maisha,
Furaha yao ni wewe kudidimia,
Na uinukapo wao hukudidimiza zaidi,
Kwa maana mafanikio yako wewe,
Huwafanya wakose usingizi usiku kucha.

Kwa maana hawawezi kulala kabisa,
Pale neema inapoyazuru maisha yako,
Ijapokuwa kupata kwako hakuwaingilii wao,
Hupenda wewe uwe chini milele na milele,
Kwa maana wao hujisikia vibaya sana,
Waionapo nuru angavu ndani ya macho yako.

Kwa maana hufikiri Mungu ni Athumani,
Wakidhani mafanikio yako yamekuja tu,
Kwamba hukuamka na kuyatafuta huko,
Hupenda kuamini kwamba wewe hustahili,
Kwa maana wao hulala tu na kusubiri,
Hujiaminisha mafanikio yatawafuata waliko.

Kwa maana wangependa mgawane taabu,
Hata kama wewe unajituma kuifukuza,
Kama vile waitamanivyo riziki hiyo yako,
Kana kwamba wewe hutafuta kwa ajili yao,
Kwa maana wao ndiyo wanaoistahili sana,
Pengine kuliko wewe mwenye kuitafuta.

Kwa maana ndivyo zinavyowatuma,
Akili zao!

No comments:

Post a Comment