Wednesday, April 4, 2007

mihela mingi mingi

haya kumekucha sasa,
sote tukaisikia mbiu hiyo,
hakuna kulala tena,
hadi kitu kieleweke,
tusije kulaumu mzee,
kwamba hakutukumbuka,
alipokuwa enzini.

sote tukasikia hiyo mbiu,
kuna mihela mingi mingi,
mzee kaimwaga kwenye benki,
kazi kwetu kuufukuza uhohehahe,
tukafurahi na kucheza ngoma,
usiku kucha tukisherehekea,
mbona raha,
udumu milele baba wa watu!

tukaingia mitaani kwa mbwembwe,
tukaanza kukopa vitu madukani,
shida ya nini wewe!
wakati kuna mabilioni kule benki,
yanayotungoja siye wajasiriamali,
tukakopa na kukopa na kukopa,
rais kamwaga mihela tutalipa tu,
siye hatuna wasiwasi bwana!

vifua mbele hadi kwa mtendaji,
naye akaringa ringa hadi tukampooza,
tukamchapa kwa noti nyekundu kadhaa,
tukazija fomu kwa madaha,
we acha tu! ni zaidi ya raha,
unapojaza fomu ya kupata milioni kadhaa,
mbona watatukoma mwaka huu!

tukazipitisha huku na kule,
hatukuona shida tulipoombwa ya soda,
zikawa tayari bwana, acha kabisa,
hatukutaka kupanda midaladala yenu,
siye hatutaki kabisa taabu bwana,
watu tuna uhakika na maisha,
wacha tujidadambwe.

mara gari yapiga breki benki,
tukashuka kwa mbwembwe zile zile,
zile za pisha tupite wenyewe bwana,
tukaikuta bonge ya foleni, usipime!
tukaambiwa ati nao wanazifuata pesa,
hawa nao!

muda ukawa unasogea, foleni haisogei,
karibu na magharibi akaja meneja,
kwa mikwara mingi,tai hapa na pale,
vijimoyo vyetu vyepesi vikakosa gavana,
akaumauma mdomo wake na kuulamba,
akasema pesa zimemalizika.

hiyo hasira almanusra nimtoe mtu uhai,
tutakwenda wapi sasa,
mbona tuliambiwa zimetolewa pesa nyingi sana?
tena zinaitwa mabilioni mengi sana,
tutaikabili vipi hali yetu ya sasa,
baada ya kuwa tumepewa matarajio mengi?

tukabaki bumbuwazi,
kumbe ahadi si mali kitu,
wala haijakidhi mahitaji halisi,
kumbe ni bora tusingeahidiwa kabisa,
kwani tusingekuwa na matarajio,
tumeponzwa na ahadi ile nzuri,
kumbe maisha bado nai magumu vile vile.

huku vichwa vikiwa chini,
tukatoka benki kwa unyonge mkubwa,
hatukutaka kupanda teksi tena,
tutaimudu vipi gharama hiyo?
na madeni nyumbani itakuwaje?
tukaumiza kichwa njia nzima,
sasa itakuwaje?

1 comment:

  1. ni kweli kabisa bwana fadhili. hizo pesa imebaki simulizi.

    ReplyDelete