Tuesday, April 17, 2007

wamezowea

kutufanya sie wajinga,
kutufanya watu tusiotambua,
tusiozitambua haki zetu ni zipi,
ni marudio ya nyakati zile,
nyakati zile zile za weupe,
japo sasa ni kwa sura mpya,
wanaona raha.

wanaofaidika na mfumo,
wamezowea kudhani wanayo sababu,
kuibinafsisha hakimiliki ya nchi,
kwani wao huona kwamba,
watu wengine si kitu sana.

husahau kuwa nyakati hupita,
kwamba hakuna aliyeiona kesho,
hutegemea matokeo ya matarajio yao,
maana huiamini nguvu yao,
wakidhani huishinda ile ya umma.

mazowea yao yamewaroga vibaya sana,
na aliyewaroga keshakufa,
tiba yao itakuwa ngumu sana,
kabla haiawadhuru kwa sana,
kwa sababu wamezowea vibaya!

vivuli vyao

ni zaidi ya mizimu ya kale,
vinatisha!
wanatamani kuvikimbia,
haiwezekani!
wana hofu kubwa hao,
nani wa kuwasaidia?
sijui!

sijui itakuwaje?
wanajiuliza daima,
na jawabu halipatikani,
kwani ni nani mwenye nalo,
zaidi yao wao wenyewe?

vinawatisha sana,
hawawezi hata kulala,
ni majinamizi ya ajabu,
ya ajabu ajabu yawajiayo,
kila siku ndotoni.

wanashindwa kumwamini mtu,
awaye yeyote yule,
kwa nini!
Aki ya ngai vile mi' wala sijui!

wanaviogopa vivuli vyao wenyewe,
vinawatishia mno amani,
lakini wanasahau kwamba,
siku yao itafika tu,
hata wangeichezea mara ngapi,
katiba ya n chi yao,

mwisho wao,unakuja tu,
watake wasitake utafika tu,
wakati ni ukuta,
zamani watu walikwishasema.

vivuli vyao vinawatisha,
Museveni hakitaki kabisa,
anakigopa kivuli chake,
Mugabe ndo wala usiseme!
haki ya Mungu siku yao ipo tu!

wanadhani wao ni zaidi ya mungu,
wanadhani wao ni zaidi ya watu!
hakika wanajidanganya!
vivuli vyao vitawatesa tu,
hata kesho na kesho kutwa,
ili wasiteseke sana,
ni heri wajitose tu leo,
kabla mambo hayajawa manbaya zaidi.

Wednesday, April 4, 2007

mihela mingi mingi

haya kumekucha sasa,
sote tukaisikia mbiu hiyo,
hakuna kulala tena,
hadi kitu kieleweke,
tusije kulaumu mzee,
kwamba hakutukumbuka,
alipokuwa enzini.

sote tukasikia hiyo mbiu,
kuna mihela mingi mingi,
mzee kaimwaga kwenye benki,
kazi kwetu kuufukuza uhohehahe,
tukafurahi na kucheza ngoma,
usiku kucha tukisherehekea,
mbona raha,
udumu milele baba wa watu!

tukaingia mitaani kwa mbwembwe,
tukaanza kukopa vitu madukani,
shida ya nini wewe!
wakati kuna mabilioni kule benki,
yanayotungoja siye wajasiriamali,
tukakopa na kukopa na kukopa,
rais kamwaga mihela tutalipa tu,
siye hatuna wasiwasi bwana!

vifua mbele hadi kwa mtendaji,
naye akaringa ringa hadi tukampooza,
tukamchapa kwa noti nyekundu kadhaa,
tukazija fomu kwa madaha,
we acha tu! ni zaidi ya raha,
unapojaza fomu ya kupata milioni kadhaa,
mbona watatukoma mwaka huu!

tukazipitisha huku na kule,
hatukuona shida tulipoombwa ya soda,
zikawa tayari bwana, acha kabisa,
hatukutaka kupanda midaladala yenu,
siye hatutaki kabisa taabu bwana,
watu tuna uhakika na maisha,
wacha tujidadambwe.

mara gari yapiga breki benki,
tukashuka kwa mbwembwe zile zile,
zile za pisha tupite wenyewe bwana,
tukaikuta bonge ya foleni, usipime!
tukaambiwa ati nao wanazifuata pesa,
hawa nao!

muda ukawa unasogea, foleni haisogei,
karibu na magharibi akaja meneja,
kwa mikwara mingi,tai hapa na pale,
vijimoyo vyetu vyepesi vikakosa gavana,
akaumauma mdomo wake na kuulamba,
akasema pesa zimemalizika.

hiyo hasira almanusra nimtoe mtu uhai,
tutakwenda wapi sasa,
mbona tuliambiwa zimetolewa pesa nyingi sana?
tena zinaitwa mabilioni mengi sana,
tutaikabili vipi hali yetu ya sasa,
baada ya kuwa tumepewa matarajio mengi?

tukabaki bumbuwazi,
kumbe ahadi si mali kitu,
wala haijakidhi mahitaji halisi,
kumbe ni bora tusingeahidiwa kabisa,
kwani tusingekuwa na matarajio,
tumeponzwa na ahadi ile nzuri,
kumbe maisha bado nai magumu vile vile.

huku vichwa vikiwa chini,
tukatoka benki kwa unyonge mkubwa,
hatukutaka kupanda teksi tena,
tutaimudu vipi gharama hiyo?
na madeni nyumbani itakuwaje?
tukaumiza kichwa njia nzima,
sasa itakuwaje?

Tuesday, April 3, 2007

wanadhani

ni rahisi kuimba wimbo wao,
ukaeleweka kwa wote,
kuna wenye vichwa vigumu,
hawaelewi kitu.

wengine ni werevu zaidi,
wanazinyaka hila,
labda kwa yule makini,
ndiye awezaye kung'amua,
na kutowa majawabu.

wamelala usingizi wa pono,
wakidhani hakutakucha,
hudanganywa nayo nuru,
ya mbalamwezi,
hawataki kuche haraka,
pengine kusiche kabisa,
jambo lisilowezekana.

hawana uwezo wa kuihimili,
miale ya nuru ya jua,
macho yao yamekufa,
ndiyo maana wao wanapenda,
kulia gizani.

wanajidanganya wenyewe,
si punde kutapambazuka,
nuru ya jua itawatesa sana,
ukali wa joto lake kuwaunguza,
watalia na nani sijui?

hakuna maji wakati huo,
wa kuyapooza maumivu hayo,
muda utakuwa umewahukumu.

wanadhani haitofika kamwe,
waache waendelee kudhani hivyo,
mbona watajiju.

wanadhani

ni rahisi kuimba wimbo wao,
ukaeleweka kwa wote,
kuna wenye vichwa vigumu,
hawaelewi kitu.

wengine ni werevu zaidi,
wanazinyaka hila,
labda kwa yule makini,
ndiye awezaye kung'amua,
na kutowa majawabu.

wamelala usingizi wa pono,
wakidhani hakutakucha,
hudanganywa nayo nuru,
ya mbalamwezi,
hawataki kuche haraka,
pengine kusiche kabisa,
jambo lisilowezekana.

hawana uwezo wa kuihimili,
miale ya nuru ya jua,
macho yao yamekufa,
ndiyo maana wao wanapenda,
kulia gizani.

wanajidanganya wenyewe,
si punde kutapambazuka,
nuru ya jua itawatesa sana,
ukali wa joto lake kuwaunguza,
watalia na nani sijui?

hakuna maji wakati huo,
wa kuyapooza maumivu hayo,
muda utakuwa umewahukumu.

wanadhani haitofika kamwe,
waache waendelee kudhani hivyo,
mbona watajiju.