Saturday, March 31, 2007

'ndiye mfano'

watu wote tumekusanyika,
na vikundi vya ngoma vikitumbuiza,
nyimbo zilizojaa ujumbe,
tunafurahi kikwelikweli,
hata na wenzetu wa mbali,
wanatamani wangehudhuria nao,
ili wapate jambo la kusimulia.

mbele yetu kuna mgeni,
ni mgeni wa heshima kweli kweli,
ametoka kule wizarani,
kunakotengenezwa sera,
amekuja na gari zuri sana,
sote tunalifurahia gari lake,
walau kwa siku moja tu,
tunasahau shida yetu ya usafiri,
gari la mzee linatufanya tujisikie raha,
ijapokuwa hatulipandi,
hata kidogo.

mgeni anatoa hotuba nzuri sana,
nasi hatuchoki kupiga makofi,
kila baada ya maneno mawili,
awali ya yote,
mgeni anavisifia vikundi vile,
vilivyotumbuiza kwa ngoma za asili,
anasema vinafaa sana kusikilizwa,
wanavikundi wapata vichwa vikubwa,
kumbe hawajui kwamba,
nyumbani kwake mzee,
kumejaa santuri za muziki wa kisasa,
kwa sababu hana muda,
na muziki wenu wa asili.

mgeni anamaliza hotuba,
na kujitolea mapesa mengi sana,
anayarusha juu kwa mbwembwe nyingi,
nasi tunagombania,
mzee anatutuliza tusiumizane,
anasema zipo nyingi tu,
zote ni kwa ajili yetu.

kumbe tena naambiwa,
ana ndugu zake wala hawajali,
wengine kijijini hawaendi shule,
kwa kukosa karo na vifaa vingine,
na mheshimiwa hatoi msaada kabisa,
ni ndugu zake wa damu hao.

mimi namkatalia mpashaji habari wangu,
haiwezekani mzee akawa hivyo,
mbona anaonesha ana roho nzuri sana?
nikajibiwa eti nitajiju,
kwa uvivu wangu wa kufikiri.

mzee akamaliza kwa kuchangia ujenzi,
wa kanisa na shule na tena msikiti,
na bomba la kumwaga maji usiku na mchana,
na barabara ataweka kokoto,
akatuahidi hivyo,
kumbe mzee anatupenda sana!
nikawaambia hao masikini wenzangu,
wakaniambia eti mimi ndiye masikini zaidi,
hawakuishia hapo,
wakasema ni masikini wa mali na akili pia.

wakaniuliza mara ya mwisho,
ni lini nilipomwona mzee kijijini pale?
ndipo nami nikafikiri kwa makini,
mama yangu!
kumbe ni miaka mitano nyuma!

nikagundua sababu ya ujio wake,
na sababu ya kutoa pesa nyingi sana,
nikawaambia hao wenzangu,
mimi ni masikini wa mali,
lakini kamwe sitokuwa masikini wa akili.

kwamba mimi hatonipata ng'oo!
atajiju yeye mwenyewe,
wenzangu wote wakacheka,
wakatamani somo lingeeleweka kwa wote,
nikawaambia wasiwe na wasiwasi,
kwa sababu 'wewe'
utawaelimisha na wengine.

No comments:

Post a Comment