Monday, March 26, 2007

kweli eeh?

wenye macho hawakuambiwa kitu,
kwani walijionea wao wenyewe,
na waliojaaliwa masikio,
waliyasikia haya kabla yangu,
nisingekuwa na jipya kwao,
tangu lini?

wengine wakadhani kwa utashi wao,
wakidhani hao hawatogutuka kamwe,
kwa sababu wanapenda daima iwe hivyo,
hawafahamu sisimizi humuua tembo,
wanacheka!

kwa kuwa wamezowea hivyo,
si tu dharau bali hata kebehi,
kana kwamba ni wao peke yao,
wenye leseni kumilikishwa hiyo,
tuliyomo nasi ndani yake.

wanajisahau sana!
wakidhani jua huwaka siku nzima,
ama labda wa juu hungojwa chini,
ilhali wao hawashuki kamwe.

wameisikia sana sauti wakauchuna,
na masikioni mwao wanazidi kuweka pamba,
wanatuona lakini hawajali,
maana karaha yetu ni raha yao,
wamepotoka!

wamepotoshwa na ndoto za kale,
wamepotoshwa na fikra zao mgando,
wanadhani dhana potofu tupu,
tupu!

hawaitamani eti kesho ifike,
wanayo nguvu ya kushindana na muda,
wanasahau kwamba wakati ni ukuta,
labda wao ni majemedari wa vita,
wenye uwezo wa kupigana na muda,
na kwamba watashinda.

ndivyo wanavyoamini wao,
na tusubiri tuone!

No comments:

Post a Comment