Saturday, March 31, 2007

'ndiye mfano'

watu wote tumekusanyika,
na vikundi vya ngoma vikitumbuiza,
nyimbo zilizojaa ujumbe,
tunafurahi kikwelikweli,
hata na wenzetu wa mbali,
wanatamani wangehudhuria nao,
ili wapate jambo la kusimulia.

mbele yetu kuna mgeni,
ni mgeni wa heshima kweli kweli,
ametoka kule wizarani,
kunakotengenezwa sera,
amekuja na gari zuri sana,
sote tunalifurahia gari lake,
walau kwa siku moja tu,
tunasahau shida yetu ya usafiri,
gari la mzee linatufanya tujisikie raha,
ijapokuwa hatulipandi,
hata kidogo.

mgeni anatoa hotuba nzuri sana,
nasi hatuchoki kupiga makofi,
kila baada ya maneno mawili,
awali ya yote,
mgeni anavisifia vikundi vile,
vilivyotumbuiza kwa ngoma za asili,
anasema vinafaa sana kusikilizwa,
wanavikundi wapata vichwa vikubwa,
kumbe hawajui kwamba,
nyumbani kwake mzee,
kumejaa santuri za muziki wa kisasa,
kwa sababu hana muda,
na muziki wenu wa asili.

mgeni anamaliza hotuba,
na kujitolea mapesa mengi sana,
anayarusha juu kwa mbwembwe nyingi,
nasi tunagombania,
mzee anatutuliza tusiumizane,
anasema zipo nyingi tu,
zote ni kwa ajili yetu.

kumbe tena naambiwa,
ana ndugu zake wala hawajali,
wengine kijijini hawaendi shule,
kwa kukosa karo na vifaa vingine,
na mheshimiwa hatoi msaada kabisa,
ni ndugu zake wa damu hao.

mimi namkatalia mpashaji habari wangu,
haiwezekani mzee akawa hivyo,
mbona anaonesha ana roho nzuri sana?
nikajibiwa eti nitajiju,
kwa uvivu wangu wa kufikiri.

mzee akamaliza kwa kuchangia ujenzi,
wa kanisa na shule na tena msikiti,
na bomba la kumwaga maji usiku na mchana,
na barabara ataweka kokoto,
akatuahidi hivyo,
kumbe mzee anatupenda sana!
nikawaambia hao masikini wenzangu,
wakaniambia eti mimi ndiye masikini zaidi,
hawakuishia hapo,
wakasema ni masikini wa mali na akili pia.

wakaniuliza mara ya mwisho,
ni lini nilipomwona mzee kijijini pale?
ndipo nami nikafikiri kwa makini,
mama yangu!
kumbe ni miaka mitano nyuma!

nikagundua sababu ya ujio wake,
na sababu ya kutoa pesa nyingi sana,
nikawaambia hao wenzangu,
mimi ni masikini wa mali,
lakini kamwe sitokuwa masikini wa akili.

kwamba mimi hatonipata ng'oo!
atajiju yeye mwenyewe,
wenzangu wote wakacheka,
wakatamani somo lingeeleweka kwa wote,
nikawaambia wasiwe na wasiwasi,
kwa sababu 'wewe'
utawaelimisha na wengine.

wanajisahau

wawapo madarakani,
husahau kuna mwisho,
ndipo hawawi makini,
hawajui kuna kesho.

hudhani watatawala,
milele yote milele,
hujikuta wanakula,
ile keki yetu yote.

wala hawana nafasi,
kuwaachia wengine,
wana tamaa ya fisi,
wale wao si wengine.

mwisho wao unakuja,
muda si mrefu sana,
inakuja siku moja,
mwisho wa hao mabwana.

Wednesday, March 28, 2007

nini zaidi?

unachokitaka sasa,
ambacho hukukivuna awali,
utakachokifanya sasa,
ambacho hukukifanya awali.

utakachowafanyia watu wako,
ambacho pengine ulikisahau,
kwambna wategemee mambo mapya,
kutoka katika kichwa cha awali,
kwamba hakuna mwingine,
afaaye,
zaidi yako wewe!

wanaopenda mabadiliko,
wanaumizwa sana nawe,
waamini nini juu ya usawa,
na haki za raia?
nini zaidi wakitegemee kwako,
zaidi ya manyanyaso unayowapa?

muda siku zinakwenda tu,
na hazitegemei kurudi tena,
hakuna jipya toka kwako,
hakuna la kujivunia kwa sasa,
nini zaidi?

awali tulikusifu kwa sana,
tukataka uwe mfano kwa wengine,
jinsi ulivyokuwa ukitijali,
kabla hujapata kiburi kichwani.

nini zaidi babu mugabe?
ili tukuelewe,
ili tusikuhukumu bure tu,
pengine unalo jambo la ziada,
tuambie basi babu yetu,
nini zaidi unachokitaka.

kama kutawala ushatawala sana,
kama ubabe ushaufanya sana,
kama mavuno ushayavuna sana,
kama nini sijui,
uhshapata kwa sana,
sasa labda tukuulize,
nini zaidi?

Monday, March 26, 2007

tupo pamoja

tupo sote pamoja,
tunajenga kwa pamoja,
na kama itabomoka,
sote tunahusika.

kweli eeh?

wenye macho hawakuambiwa kitu,
kwani walijionea wao wenyewe,
na waliojaaliwa masikio,
waliyasikia haya kabla yangu,
nisingekuwa na jipya kwao,
tangu lini?

wengine wakadhani kwa utashi wao,
wakidhani hao hawatogutuka kamwe,
kwa sababu wanapenda daima iwe hivyo,
hawafahamu sisimizi humuua tembo,
wanacheka!

kwa kuwa wamezowea hivyo,
si tu dharau bali hata kebehi,
kana kwamba ni wao peke yao,
wenye leseni kumilikishwa hiyo,
tuliyomo nasi ndani yake.

wanajisahau sana!
wakidhani jua huwaka siku nzima,
ama labda wa juu hungojwa chini,
ilhali wao hawashuki kamwe.

wameisikia sana sauti wakauchuna,
na masikioni mwao wanazidi kuweka pamba,
wanatuona lakini hawajali,
maana karaha yetu ni raha yao,
wamepotoka!

wamepotoshwa na ndoto za kale,
wamepotoshwa na fikra zao mgando,
wanadhani dhana potofu tupu,
tupu!

hawaitamani eti kesho ifike,
wanayo nguvu ya kushindana na muda,
wanasahau kwamba wakati ni ukuta,
labda wao ni majemedari wa vita,
wenye uwezo wa kupigana na muda,
na kwamba watashinda.

ndivyo wanavyoamini wao,
na tusubiri tuone!

wewe ungesemaje?

wewe ungesemaje?

pale unapohitaji mabadiliko,
pale unapohitaji haki yako,
ungeipazaje hiyo sauti yako?
ili isikike hata kwa wenzako?

wewe peke yako ungeweza,
kama wenzako usingewajuza?
unadhani yasingekutatiza,
kama wewe usingejifunza?

ni vema kama ungeshiriki,
wewe na wako wema marafiki,
kuitoa nchi yetu kwenye dhiki,
kwenye dhiki kubwa ya haki!

ni nchi yako simama uipiganie,
na wenzako wengine wakusaidie,
ili sote kwa pamoja tuifikie,
haki sawa ili tuifurahie.

hakika tunapaswa kwa hakika.