Friday, March 31, 2017

N'wapi?

Menihifadhia penzi,
Lije nitoe simanzi,
N'wapi eeh laazizi,
Mwenzio nakungojea.

N'wapi hebu nambie,
Liliko nilif'atie,
Tangu moyoni 'nijie,
Siwachi kukuwazia.

N'wapi umelificha,
Nalingoja usiku kucha,
Moyoni napata "torture",
Mawazo yanizidia.

Nimezama nimezama,
Moyo wangu kutuwama,
Sikia ninavyohema,
Moyo wenda peapea.

N'wapi huko uliko,
Niambie neno lako,
Lenye haki si zindiko,
Moyo upate tulia.

Nikilala nakuota,
Kwani lini nakupata?
Wajua kwako 'megota,
Wataka mie ugua?

N'wapi nikufuate?
N'fanyeje nikupate?
N'wapi mi' nikukute?
Moyo'ngu wataka jua.

Fadhy Mtanga,
Mbeya,  Tanzania.
Ijumaa, Machi 31, 2017.

Tuesday, March 28, 2017

Vile Ulivyo

Vile we' utembeavyo,
Kwa mikogo,
Ndivyo univutiavyo,
Si kidogo.

Vile unitazamavyo,
Ooh walah!
Ndivyo unimalizavyo,
Mie hoi.

Na rangi yako ilivyo,
Asilia,
Kwa namna ing'aavyo,
Yavutia.

Vile neno usemavyo,
Shamshamu,
Sauti ikutokavyo,
Kwa utamu.

Umbo zuri vivyo hivyo,
Mashaallah!
Linoge vile wendavyo,
Inshaallah.

Hata hivi nandikavyo,
Kwa utenzi,
Ndo hivyo nikuwazavyo,
Sijiwezi.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Jumanne, Machi 28, 2017.

Sunday, February 19, 2017

Our Pain

Your pain,  yet more my pain,
Aliandika Armando Guebuza,
Sasa kimewakumba kitu gani,
Hata kwenu mwatufukuza?

Your pain,  yet more my pain,
Tulifundishwa hadi shuleni,
Maumivu  mwenu mioyoni,
Yakawa yetu pia nchini.

Your pain,  ikawa yetu pain,
Kamwe hatukuwaacha nyuma,
Tulihamasishana nchini,
Kilimanjaro hadi Kigoma.

Your pain,  ilijaa hisia,
Sauti kali ya Kiafrika,
Yeyote iliyemfikia,
Hakika alihamasika.

Kusini kwa mto Ruvuma,
Tulijua mwateseka,
Tukawapa ofisi Nkrumah,
Ili mipango kupangika.

Our pain, never your pain,
Leo hii mwatufukuza?

Fadhy Mtanga,
Njombe.
Jumamosi, Februari 18, 2017

Friday, October 28, 2016

Waulizeni

Waulizeni watu wale,
Na wasilale,
Wakumbusheni siku zile,
Na mambo yale,
Kama ni chakula wakile,
Wasijali hata kama cha wale,
Maana ni yale yale!

Mnaandika lakini?

Waulizeni kwa yakini,
Wafikiri vichwani,
Tangu lini?
Iliwajia machoni,
Ile namba ya mwanzoni,
Ikawa asalini,
Tangu lini?

Ama kumekucha?

Hauchi hauchi wecha,
Wavichachuavyo vimechacha?
Ye wapi yenu mapakacha,
Kumekucha na makucha,
Si asali bali ‘tocha’,
Waulizeni pasi kuacha,
Hata neno msijeficha.

Watasema kweli?

Lanipa shaka shauri hili,
Kama watalihimili,
Yaone macho yao mawili,
Na mioyo yao ikubali,
Kuwa kuna kufeli,
Ama kufaulu asilimia mbili,
Basi, msiulize tena maswali.

Fadhy Mtanga,
Mbeya.

Ijumaa, Oktoba 28, 2016.

Saturday, July 9, 2016

Uzuri wako

Uzuri wako wewe unanipa kiwewe,
Nifanye nini mie ili niwe na wewe?
Mi si Mr Nice wimbo uimbiwe,
Wewe ukadhani aimbiwa mwinginewe, 
Lahaulah!

Moyo wangu umeujaza tele hisia,
Namna siku z'endavyo nazo zazidia,
Kukufahamu wewe mie najivunia,
Wanipa raha maisha kuyafurahia,
Alhamdulillah!

U mzuri mwenye macho mithili ya hua,
Kila niyaonapo nahisi kuugua,
Nina raha u tabibu unayenijua,
Nami najivunia wewe kukuchagua,
Ewaaaaaaah!

Rangiyo yavutia toto rangi rangile,
Rangi ivutiapo, yang'ara naturally,
U msichana mrembo zako sifa tele,
Wan'ache nikusifie kwa vigelegele
Mashaallah!

Unayo sauti utadhani ya kinanda,
Ama ya ndege tena yule angali kinda,
Sauti iso na mawaa iso na inda,
Naitamani iniambie wanipenda,
Inshaallah!

Uzuri wako niufananishe na nini?
Ah wapi, cha kufananishia sikioni!
Waniache nikupende nizame dimbwini,
Dimbwi la mahaba kwa raha yalosheheni,
Aaaaah!

Wewe u pekee, peke yako duniani,
Katu sitosema you are my number one,
Kwa maana wewe kwangu hunacho kifani,
Sijaona kokote, kote bara na pwani,
Walaah!

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Jumamosi, Julai 9, 2016.

Friday, June 17, 2016

Tabibu

Nataka uwe tabibu,
Wala usilete gubu,
Nani alokughilibu,
Mie ukanikimbia?

Miaka mingi yaenda,
Hakiniponi kidonda,
'Lisema hutonitenda,
Nini kikaja tokea?

Ulisema utabaki,
Penye raha ama dhiki,
Ghafla 'katoka nduki,
Simanzi kuniachia.

Ni wapi huko uliko,
Nikuf'ate hukohuko,
Hadi n'fanye zindiko,
Ndipo utaporejea?

Nambie nifanye nini,
Tuishi kama zamani,
'Siseme mwako moyoni,
Eti 'lishaniondoa.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Ijumaa, Juni 17, 2016.

Wednesday, June 15, 2016

Nimeuona Uzuri Wako

Nimeuona uso wa kirembo hasa,
Kidevu kivutiacho kukitazama na kukishika,
Macho mazuri mithili ya njiwa mpole,
Yanayoleta raha sana moyoni kuyatazama,
Yakisindikizwa na nyusi chache nyeusi,
Nimeiona pua ndogo ikidhiyo haja ya urembo,
Juu ya midomo mipana,
Yenye kuvutia,
Iletayo hamu kuishuhudia ikifunguka,
Kwa kuongea ama mengineyo,
Rangi ya mwili inayong'ara isivyo kifani,
Mabega laini yakaribishayo,
Hamu ya kukiweka kichwa juu yake,
Huku masikio yakiwa tayari,
Kuyapokea maneno matamu yaburudishayo moyo,
Nimeuona uzuri wako,
Ila maneno hayatoshi kuuelezea.

U mzuri miongoni mwao,
Waliojaaliwa uzuri wa haja!

Friday, May 13, 2016

Wewe huyo!

Nikiutafakari,
Ukwasi wa dahari,
Kwa kadri,
Nyakati zinavyojiri,
Oooh u johari.

Kamwe hujui shari,
Mahiri.

Beti za mashairi,
Zadhihiri,
Hunayo nambari,
Wa pekee kwenye sayari.

Oooh u johari,
Kwa ukwasi wa dahari.

Moyoni washamiri.

Oooh u johari,
Moyoni wanipa fahari.

Hunayo nambari,
U mkwasi wa dahari,
Oooh kwangu u sayari.

Fadhy Mtanga,
Tanangozi, Iringa.
Ijumaa, Mei 13, 2016.

Sunday, May 8, 2016

Ninyunyizie

Ninyunyizie,
Nami ninukie,
Harufu iwafikie,
Wivu uwazidie,
Donge liwapalie.

Wenye husda walie.

Wenye ngebe waumie.

Ngendembwe ziwaishie.

Ninyunyizie,
Nizidishie.

Marashi ya upendo.

Fadhy Mtanga,
Mafinga, Iringa.
Jumapili, Mei 8, 2016.

Thursday, January 14, 2016

Nataka Chai

Siyo iliyochemshwa,
Itakuwa tu mchemsho,
Itanichemsha!

Nataka iliyopikwa,
Bonge la mpiko,
Ikapikika.

Tena kwa ufundi,
Siyo ufundoo,
Ikafundika.

Nataka yenye utamu,
Siyo tamutamu,
Bali tamu kolea.

Hadi kisogoni!

Nataka yenye viungo,
Siyo uongo uongo,
Weka masala,
Yafate hata Salasala!
Yatangulizie sala.

Nataka chai mie,
Nna kiu nayo!

Iweke kila kitu,
Mdalasini,
Tangawizi,
Pilipili manga,
Majani yake,
Sukari usiisahau.
Ukiweza,
Weka asali.

Niweke mezani,
Meza safi,
Iliyosafishwa,
Ikasafishika.

Chai kikombeni,
Nataka kikombe kimoja tu,
Na mshikio wake moja,
Kikombe cheupe,
Kiso na doa.

Nataka chai,
Ndashene!

Chai tamu,
Tamu yenye utamu,
Utamu mtamu,
Utamu kolea.

Nataka chai miye!

Usininyime mwanakwetu!

Lakini,
Sinipe yenye kuunguza,
Wangu ulimi.

Fadhy Mtanga,
Chole Road, Masaki, Dar es Salaam.
Alhamisi, Januari 14, 2016.

Thursday, December 31, 2015

Mwaka UnapokwendaKumbe mwaka unakwisha,
Kalenda yaniambia,
Mwaka unapokwenda,
Basi uende peke yake,
Usiende na mapenzi yangu,
Usiende na furaha yangu.

Miezi kumi na mbili,
Ina mengi sana,
Siku mia tatu sitini na tano,
Basi ziende peke yake,
Zisiende na mapenzi yangu,
Zisiende na furaha yangu.

Wiki zimekatika katika,
Zikaenda zake,
Wiki hamsini na mbili,
Basi ziende peke yake,
Zisiende na mapenzi yangu,
Zisiende na furaha yangu.

Maisha lazima yaendelee,
Chambilecho wahenga,
Zichanike jamvi zivunjike koleo,
Basi viende peke yake,
Visiende na mapenzi yangu,
Visiende na furaha yangu.

Nenda mwaka nenda zako,
Ewe mwaka nenda zako,
Lakini unapokwenda,
Basi uende peke yake,
Usiende na mapenzi yangu,
Usiende na furaha yangu.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Alhamisi, Disemba 31, 2015.

Thursday, December 3, 2015

Mpenzi kalamu

Salamu,

Ee wangu muhashamu,
Ulo kwangu muhimu,
Tena daima dawamu,
Aaah wanipa raha!

Niliitupa zamu,
Kisa eti majukumu,
Ni nini huu wazimu,
Aaah mbona karaha!

N'sharejea mumu humu,
N'shaitema ile sumu,
Wewe u wangu mwalimu,
Aaaah mbona furaha!

Mpenzi wangu muhimu,
Mpenzi wangu kalamu,
Niondolee magumu,
Aaaah nipate siha!

Pokea zangu salamu!

Fadhy Mtanga,
Tukuyu, Mbeya.
Alhamisi, Disemba 3, 2015.

Wednesday, July 1, 2015

Oooh!

Kijana!
Mwanakwetu una nini, nauliza,
Ni nani kakurubuni, waniliza,
Umepatwa mashetani, nguvu giza?
Wanishangaza!

Kijana!
Shuleni umekwenda, umesoma,
Twangojea matunda, yalo mema,
Na siyo yaliyovunda, tukatema,
Kijana wewe!

Kijana!
Watetea mafisadi, kisa pesa,
H'wambiliki kaidi, tele visa,
Tena wafanya kusudi, umenasa,
Huna maana!

Vijana!
Eti mnazo timu, hovyo hovyo,
Mnajitia wazimu, mfanyavyo,
Muda utawahukumu, nionavyo,
Mnatumika!

Vijana!
Timu nao marafiki, mmekwisha,
Wala hamueleweki, mwatuchosha,
Na tena hatuwataki, mwapotosha,
Nchi si yenu!

Wenzangu!
Na msituchagulie, hatutaki,
Na msitusafishie, kwayo jiki,
Nyie mumtumikie, ni rafiki,
Ila si kwetu!

Wenzangu!
Historia huhukumu, ilisemwa,
Na maandishi hudumu, yakasomwa,
Msitupe sie sumu, tukaumwa,
Wala si sawa!

Wananchi!
Oktoba ikifika, tujihimu,
Kura zetu kuziweka, ni muhimu,
Tuchague kwa hakika, muashamu,
Kutuongoza!

Wananchi!
Ni vema tudhamirie, kwazo nia,
Makosa tusirudie, tutalia,
Kwa busara tuchague, Tanzania,
Atufaaye!

Wananchi!
Wito wangu nautoa, kwa yamini,
Mola azidi jalia, taifani,
Uchaguzi 'kifikia, umakini,
Chaguo bora!

Fadhy Mtanga,
Kihesa, Iringa.
Alhamisi, Julai 2, 2015.

Friday, August 15, 2014

Nayapenda maisha

Nayapenda maisha,
Kwa furaha yanipayo,
Kwa huzuni yanileteayo.

Nayapenda maisha,
Kwa mapenzi niyapatayo,
Kwa chuki zinipitiazo.

Nayapenda maisha,
Kwa mafanikio nipatayo,
Kwa changamoto nizipatazo.

Nayapenda maisha,
Kwa jitihada nilizonazo,
Kwa uvivu niupatao.

Nayapenda maisha,
Kwa ndugu wema nilionao,
Kwa ndugu wanichukiao.

Nayapenda maisha,
Kwa marafiki wema niwapatao,
Kwa wanafiki watokeao,

Nayapenda maisha,
Kwa afya njema niliyonayo,
Kwa maradhi yanipitiayo.

Nayapenda maisha,
Kwa akili nilizonazo,
Kwa umbumbumbu nilionao.

Nayapenda maisha,
Kwa imani na dini niliyonayo,
Kwa kutikiswa nikupitiako.

Nayapenda maisha,
Kwa maono na dhamira niliyonayo,
Kwa kukata tamaa nisikokuwa nako.

Nayapenda maisha.

Nayapenda sana.

Fadhy Mtanga,
Kabwe, Mbeya.
Ijumaa, Agosti 15, 2014.

Saturday, June 28, 2014

Wewe huyo

Unang'ara mwangu machoni,
Wachanua mwangu moyoni,
Niende kote duniani,
Sitoona chako kifani,
Nikupende wewe tu,
Ndivyo moyo wanambia!

Nasema yangu ya moyoni,
Kuficha siwezi jamani,
Nimezama mie dimbwini,
Nimezama mi mapenzini,
Mahaba nivuruge tu,
Moyo wangu wafurahia!

Nivuruge tu hak'ya nani,
Mahaba nijaze rahani,
Nikoleze hadi moyoni,
Nikoroge mwangu kichwani,
Unijaze mahaba tu,
Nifurahi na dunia!

Unibusu pangu shavuni,
Na mpapaso mgongoni,
Ninong'oneze sikioni,
Kwa sauti yako laini,
Nakutamani wewe tu,
Ambaye kwako nimetua!

Furaha yangu duniani,
N'sahaulishe ya zamani,
Maumivu siyatamani,
We ndo tabibu wa thamani,
Unanimudu wewe tu,
Juu yako nayeugua!

Umetamalaki moyoni,
Unatawala mawazoni,
U mwenza wangu duniani,
Na rafiki yangu ndotoni,
Wacha nikuwaze wewe tu,
Ndicho nachokifurahia!

Fadhy Mtanga,
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Jumamosi, Juni 28, 2014.

Friday, March 28, 2014

Tumerogwa?

Dziseketa mwileme!

Kwa makuhani, wanaohani na makuhana,
Waugeuzao usiku kwa hila ili uwe mchana,
Waso haya, waso sudi wawazao tu kutukana,
Wasojali na kuzijali walizopewa hizo dhamana,
Wadhaniao wao ndo wa leo ilhali zetu fikra za jana,
Bado tukawaamini tukawaambia tena na tena,
Tumerogwa?

Tabibu?
Kwao weledi walokubuhu vichwani pengine kwa funza,
Wenye mang'onyo wakalewa misasati vichwani wakateleza,
Watuaminishao kwa yao matingo kichwa kichwa tukajiingiza,
Tumepotea, tumepotezwa, tumepotezana ama tumepoteza?
Kaa? Tiba? Yaliapo mbwata kwa ushambenga muda tukipoteza,
Twajiona sisi ndo kitu na kilakitu sisi ndo tunaweza,
Tumerogwa!

Fadhy Mtanga,
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Ijumaa, Machi 28, 2014

Tuesday, December 3, 2013

Ya'ani?

Hino si sino yaani, siy’echi yalo ngamani,
Neno ndilo mdomoni, waama sina utani,
Ushanijaa moyoni, sifurukuti yaani,
Ya’ani kuficha?

Siyo mboni ‘lo jichoni, bali moyo ‘lo moyoni,
Maneno tupu sineni, nakutenda yalo shani,
Meshiba mie pendoni, nakupendaje yaani,
Ya’ani kuficha?

Vijinopembe pembeni, yawachome mioyoni,
Nishazama ‘mo rahani, nilotopea dimbwini,
Dimbwini ‘ko mahabani, mbona ‘na raha
yaani,
Ya’ani kuficha?

Jamani mie jamani, msin’ulize ‘na nini,
Nimependa duniani, sisikii ‘la sioni,
Guuni ‘di utosini, sijielewi yaani,
Ya’ani kuficha?

Kote kote duniani, mwingine ‘tomtamani,
Nitataka tena nini, na sitaki abadani,
Nihangaike kwa’ani, basi n’wehuke yaani,
Ya’ani kuficha?

Mlo na gere oneni, mgae gae upwani,
Zino kavu mtaleni, mu’nge wajihi puani,
Nimependa niwacheni, nijinomee yaani,
Ya’ani kuficha?

Sifichani ‘mo nenoni, utamuwe ‘so kifani,
Yaani!

Fadhy Mtanga,
Mtongani, Dar es Salaam.
Jumanne, Disemba 3, 2013.

Tuesday, October 1, 2013

Jivute taratibu

Mpenzi sogea ujivute taratibu,
Haya maradhi ya moyo uje kuyatibu,
Njoo unibembeleze ukiwa karibu,
Ewe nikupendaye ulo wangu muhibu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Njoo karibu nikweleze yanonisibu,
Nikueleze ewe ulo wangu tabibu,
Unipozaye yanijiapo masahibu,
Mapenzi unipayo yenye nguvu ajabu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Mpenzi wangu wang'ara kuzidi dhahabu,
Mpenzi wanukia nukato mahabubu,
Tunu nakupatia kwa moyo kuratibu,
Wewe ndo wangu hunacho kifani taibu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Ukiniacha moyo utapata taabu,
Nichanganyikiwe nikose hata adabu,
Nijaze mapenzi tena bila kuhesabu,
Wewe kukuacha katu siwezi jaribu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Mapenzi unipayo tuzo yako thawabu,
Kwako nimezama mapenzini nimeghibu,
Nikikosa nambie sitosita kutubu,
Usininunie mapenzi tukaharibu,
Jivute taratibu, sogea karibu.

Fadhy Mtanga,
Morogoro.
Jumanne, Oktoba 1, 2013.

Thursday, September 12, 2013

Wewe ndo furaha yangu

Wangu moyo laazizi, wewe nimekupatia,
Juu yako sijiwezi, moyo umekuchagua,
Kukupenda s’oni kazi, mwenyewe nimeridhia,
Wewe ndo furaha yangu, wanipa kutabasamu.

Sipigi tena miluzi, nukta nishaitia,
Kutangatanga siwazi, vyote we’ wanipatia,
Kwingine kwenda siwezi, hakuna ‘lokufikia,
Wewe ndo furaha yangu, mapenzi yako matamu.

We ndo wangu usingizi, daima nakuwazia,
Wanijia kwenye njozi, hakuna wa kunambia,
Moyo mejaa mapenzi, wewe nimekujazia,
Wewe ndo furaha yangu, juu yako si’shi hamu.

Siw’ogopi wazengezi, kwako nimeshatulia,
Wengine naw’ona ndezi, moyo umeshachukua,
Hayatoshi maongezi, wewe nikakusifia,
Wewe ndo furaha yangu, wa moyoni muhashamu.

Maisha yana viunzi, penzi kutuharibia,
Nabana zangu pumzi, penzi letu nalindia,
Wengine wana majonzi, kutwona twafurahia,
Wewe ndo furaha yangu, duniani kote humu.

Nayasema wazi wazi, kwako nimeshakolea,
Kwingine sikuangazi, kwako wewe nimetua,
Kukusaliti siwezi, leo ahadi  natoa,

Wewe ndo furaha yangu, ya daima na dawamu.

Fadhy Mtanga,
Sinza Mori, Dar es Salaam.
Alhamisi, Septemba 12, 2013.

Sunday, September 8, 2013

Kama nyota za angani

Kama nyota za angani,
Usiku zinavyong’aa, ndivyo penzi langu kwako,
Mapenzi yamenijaa, huba tele juu yako,
Wala sikati tamaa, mimi ndiye mali yako.

Kama nyota za angani,
Usiku zinavyong’aa, ndivyo ninavyokupenda,
Kwako mefika haswaa, kwingine siwezi kwenda,
Maneno nayakataa, yaso ubani yavunda.

Kama nyota za angani,
Usiku zinavyong’aa, wewe ndo mpenzi wangu,
Bora wakinishangaa, sitoweza peke yangu,
Kamwe sijihisi njaa, uwapo pembeni yangu.

Kama nyota za angani,
Usiku zinavyong’aa, daima nitakuenzi,
Siwezi kukuhadaa, ewe wangu laazizi,

Moyoni ushanikaa, we ndiwe wangu mpenzi.

Fadhy Mtanga,
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Jumapili, Septemba 8, 2013.